Breaking

Friday, 6 December 2024

DCEA Yaendelea na Juhudi za Kupambana na Dawa za Kulevya, Yapongezwa na Ujumbe wa Marekani

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) leo tarehe 6 Disemba, 2024 imetembelewa na Naibu Katibu Msaidizi wa Shirika la Kimataifa linaloghughulikia dawa za kulevya, ugaidi, uhalifu wa kimataifa, na masuala ya haki za binadamu (INL) Maggie Nardi, pamoja na ujumbe wake.

Ziara hiyo ililenga kutambua mafanikio ya DCEA katika kuvunja mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na kujadili ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti biashara hiyo hatari.

Akizungumza na ujumbe huo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas J. Lyimo, aliwashukuru serikali ya Marekani kwa msaada wake kupitia Shirika la Kimataifa la Dawa na Masuala ya Sheria. Msaada huu umewezesha DCEA kufanya operesheni kubwa za kukamata dawa za kulevya na wahalifu, na kuimarisha juhudi za kudhibiti dawa za kulevya nchini.

Katika kipindi cha Machi 2023 hadi Novemba 2024, DCEA imefanya operesheni mbalimbali ambazo zimefanikiwa kukamata zaidi ya tani 4,280 za dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na bangi, Mirungi, methamphetamine, heroin, na cocaine. DCEA pia imeweza kuteketeza mashamba ya bangi na mirungi na kukamata kemikali bashirifu.

Mbali na hatua za kupunguza usambazaji wa dawa za kulevya, DCEA pia inaendelea na juhudi za kupunguza matumizi ya dawa za kulevya kupitia elimu kwa jamii ambapo takribani watu milioni 25 kutoka makundi mbalimbali ya jamii, wamefikiwa na programu za elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Pia, Lyimo alielezea juhudi za DCEA katika kutoa huduma za matibabu kwa waathirika wa uraibu wa dawa za kulevya, kupitia vituo vya MAT na nyumba za matibabu. Alisisitiza pia uhusiano mzuri na Idara ya Dawa za Kulevya ya Marekani (DEA), ambao umewezesha operesheni za pamoja na kubadilishana taarifa muhimu, ikiwemo mafanikio ya kukamata na kuwakamata wahalifu wa kimataifa.

Kwa upande wake, Maggie Nardi amelezea kufurahishwa na ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya DCEA na kutoa pongezi kwa DCEA kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.

"Ninawapongeza operesheni za kukamata dawa za kulevya mlizozifanya. Mnafanya kazi nzuri na ni furaha yangu kuona kwamba tunashirikiana nanyi. Uhusiano huu ni mzuri na tungependa kuendelea kuutunza."

Pamoja na pongezi hizo Maggie pia alifurahishwa na huduma za kupunguza uhitaji ya dawa za kulevya na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya.

"Sikufahamu kwamba DCEA pia inafanya kazi ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya Pamoja na kupunguza madhara ya dawa hizo. Hii ni hatua nzuri ambayo inapaswa kuendelea," alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu tishio la dawa za kulevya, Nardi alielezea tishio linalotokana na dawa za kulevya za kisintetiki kama vile fentanyl, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na ushirikano wa habari ili kukabiliana na changamoto hii.

"Natumai fentanyl haijaingia kwa wingi hapa nchini, lakini lazima tuchukue tahadhari. Tunaendelea kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya biashara ya dawa za kulevya. Marekani ilijifunza kutokana na kile kilichotokea katika majimbo ya Kaskazini Mashariki, na hivyo walijitayarisha vyema wakati fentanyl ilipokuwa ikienea. Hii inadhihirisha umuhimu wa kushirikiana taarifa mapema." Alisisitiza Maggie.

Maggie aliahidi kuyafanyia kazi mahitaji ya DCEA na kusema kuwa watatumia kila njia kuhakikisha msaada unaendelea kutolewa .

"Tanzania pia ni mshiriki katika muungano wa kimataifa wa kupambana na vitisho vya dawa za kulevya za kisintetiki. Kupitia hilo, tunajaribu kuongeza ushirikiano wa maabara za forensiki na kufanya operesheni zaidi duniani kote."

Ziara hii ni ishara ya ushirikiano wa kimataifa unaozidi kuimarika katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, na DCEA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali ya Marekani, ili kupambana na janga hili na kupunguza athari zake kwa jamii.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages