Breaking

Saturday, 21 December 2024

CCM HATUHITAJI AHADI, TUNAHITAJI MTU MWENYE KUPAMBANIA WANANCHI WAKE - NDG. ISSA GAVU

> CCM Yakemea viongozi wenye kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na kukandamiza watu.

" Kwa mujibu wa ibara ya 16 inamtaja nani kiongozi, maana yake kiongozi ni mwanachama yeyote wa CCM aliyepewa dhamana kwa kuchaguliwa ama kuteuliwa " Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC - Idara ya Oganaizesheni wa CCM Taifa Ndugu. Issa Haji Ussi Gavu aliposhiriki akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa, mara baada ya kupokea Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM. 

Mkutano huo umefanyika leo tarehe 21 Desemba, 2024.

Akizungumza na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji Pamoja na Wajumbe na Mabalozi, Ndugu. Gavu amebainisha sifa za kumfanya kiongozi kuendelea kuongoza ambapo miongoni mwake amesema kutotawaliwa na tamaa, kutokuwa na mapato ya kificho, kutokuwa mbinafsi na kuwa tayari kusambaza matunda ya nafasi yako kuwanufaisha wananchi unaowaongoza. 

Vilevile, Ndugu. Gavu amewataka viongozi hao wa serikali za mitaa kukumbuka kuwa dhamana iliyowapa nafasi ya kugombea na kushinda ni Chama Cha Mapinduzi hivyo kuwaonya kutotumia koti la uongozi vibaya na badala yake kuwatumikia wananchi wanaowaongoza kwa kuzingatia misingi na taratibu za kiserikali. 

Aidha, Ndugu. Gavu amesisitiza juu ya viongozi kujiepusha na vitendo vya kupokea rushwa na kukandamiza watu haswa katika haki pamoja na utumiaji wa mihuli katika vitendo vya kujihusisha na wizi ama dhulma. 

Kwa upande mwingine, Ndugu. Gavu amesema kiongozi yoyote atakayejihusisha na vitendo vya wizi, dhulma ama rushwa katika kunyanyasa watu waliopiga kura kukupa dhamana hiyo basi mwenyewe aache mara moja na atatafutwa mtu mwingine katika nafasi hiyo na CCM haitasita kuchukua hatua.

"Hatuhitaji ahadi tunahitaji mtu anayeweza kupambana katika kuwatumikia watanzania waliotupa imani na matumaini yao tuyalete ndani ya chama chetu (CCM) na tukapata heshima ya kupeperusha vema bendera ya chama chetu kwa kuwatumikia kwa vitendo...kutatua changamoto " Alisema Ndugu. Gavu.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages