Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa ziara ya kukagua hatua maendeleo ujenzi wa Madaraja Halmashauri ya Ushetu Mkoa wa Shinyanga.
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Katika hatua kubwa ya kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja mkoani Shinyanga, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga kukagua na kukabidhi ujenzi wa madaraja kwa wakandarasi.
Ziara hiyo imefanyika leo Novemba 30, 2024, ambapo Waziri Bashungwa amesema Rais Samia ametenga kiasi cha shilingi bilioni 868 kwa ajili ya kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El Nino na kimbunga Hidaya kama vile barabara na madaraja.
Bashungwa amesema Halmashauri ya Ushetu imetengewa shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kukarabati wa madaraja manne yaliyoharibiwa na mvua, likiwemo daraja linalounganisha Ushetu na Geita.
Bashungwa amefafanua kuwa Halmashauri ya Ushetu inatekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja matatu yenye thamani ya shilingi bilioni 13.5 ambayo yatakamilika katika kipindi cha miezi 12, Pia daraja linalounganisha Ushetu na Geita lenye urefu wa mita 50 linalogharimu shilingi bilioni 5.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja, akisema kuwa wananchi wa Ushetu walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa kutokana na hali mbaya ya miundombinu.
Macha amesema shughuli zote za maendeleo zinaunganishwa na ujenzi wa miundo mbinu ya barabara hivyo ataendelea kuwafuatilia wakandarasi mpaka miradi ikamilike, pia wananchi waitunze miradi hiyo na kuwa waaminifu kwa kulinda vifaa vyote vya ujenzi.
Aidha Macha amewaasa wananchi kulinda afya zao kwani ugonjwa wa UKIMWI upo na unaua hivyo miradi yote inayofanyika pasipo afya haiwezi kuwa kitu
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ameelezea furaha ya wananchi, akisema kuwa serikali imejibu kiu yao ya muda mrefu ya kujengwa kwa madaraja ambayo yatakuwa na manufaa makubwa katika shughuli za kiuchumi na usafiri.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambungu akitoa taarifa ya ujenzi wa Madaraja Ushetu.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samweli Mwambungu, ametoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mikataba ya ujenzi wa madaraja hayo, akisema kuwa kazi zitakamilika ndani ya miezi 12 na madaraja yatakamilika kwa ubora.
Wakandarasi kutoka Kampuni ya Salum Motor Transport Limited, wanaotekeleza mradi wa daraja la Ubagwe, wameahidi kuwa mradi huo utazingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa muda wa mkataba.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Ushetu Martha Shija ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto ya madaraja kwani walikuwa wanapata shida wakati wa masika barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na maji mengi hivyo ujenzi huo utarahisisha mawasiliano na vijiji jirani.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara na wananchi wa Ushetu katika Kijiji cha Bugomba.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kahama Thomas Muyonga akizungumza kwenye mkutano huo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza katika ziara hiyo.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza na Wakandarasi ambao wanajenga daraja la Ubagwe.
Daraja ambalo wanapita wananchi wa Ubagwe ambalo litafanyiwa ukarabati mkubwa na kuwa daraja la kudumu.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa wa pili (katikati) akiwasili Bugomba Halmashauri ya Ushetu.
Picha na MARCO MADUHU