Breaking

Wednesday, 6 November 2024

TET, SOMA KWANZA Washirikiana Kuboresha Elimu kwa Teknolojia

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)kwa kushirikiana na wadau kutoka Soma Kwanza wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kuboresha Sekta ya Elimu nchini ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora na yakidijitali.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 6/11/2024  na Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Soma Kwanza Bw. Peter Kangere na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Taasisi hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mkurugenzi Mkuu wa  TET, Dkt. Aneth Komba amesema, malengo makuu ya makubaliano yaliyosainiwa ni kuimarisha na kuendeleza sekta ya elimu nchini kupitia kuandaa  vifaa na miundombinu ya kidigitali itakayosaidia kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema,  Soma Kwanza wataanzisha televisheni, redio, na programu (apps) kwa jina la TIE – Soma Kwanza Television vitavyosaidia kuchochea ujifunzaji na ufundishaji katika Sekta ya Elimu nchini.

Ameongeza  kuwa, kwa pamoja watashirikiana kuwezesha upatikanaji wa miundombinu (vifaa, utaalam, na rasilimali fedha), huku TET ikiratibu upatikanaji wa wataalamu wa ufundishaji wa teknolojia za elimu (Educational technologies) katika shule za serikali, mijini na vijijini.

Pia , amesema kuwa katika Mitaala iliyoboreshwa Serikali imeimarisha matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine katika ufundishaji na ujifunzaji, hivyo matumizi ya TEHAMA yamechopekwa  katika  vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji katika masomo yote kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu kutoka SOMA KWANZA Bw. Peter Kangere amesema, SOMA KWANZA itaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuhakikisha watoto wa Tanzania hawatabaki nyuma katika mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea Duniani. 

Sambamba na hilo Bw. Kangere amesema, maudhui ya Elimu yatayokuwa yakitolewa katika televisheni, redio na programu za TIE - SOMA KWANZA yatawiana na Mtaala ulioboreshwa ili wanafunzi kutoka pande zote wapate Elimu yenye ubora na kwa njia rahisi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages