Breaking

Thursday, 21 November 2024

TANAPA Yatoa Pole na Msaada wa Milioni 20 kwa Wahanga wa Ajali ya Ghorofa Kariakoo

MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara akiongozana na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji, leo tarehe 21, Novemba 2024 wameungana na watanzania kutoa pole kwa wahanga wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa - Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

“TANAPA, kwa masikitiko makubwa inaungana na jumuiya za wafanyabiashara na watanzania wote kutoa pole kwa wafanyabiashara wa Kariakoo waliofikwa na ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa,ndugu zetu waliopoteza maisha katika ajali hii tunawaombea wapumzike kwa amani, na majeruhi wapone haraka ”. Alisema Jenerali Waitara.

Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na Watumishi wote wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali Waitara amekabidhi hundi ya malipo ya kiasi cha shillingi Millioni 20 kwa Dkt. Jim James Yonazi Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ikiwa ni pole kwa wahanga wa ajali hiyo ya kusikitisha ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa.

Katibu Mkuu Dkt.Yonazi, aliishukuru TANAPA kwa namna ambavyo imeguswa na kushirikiana na wananchi katika kutoa pole na kurejesha hali ya wananchi.

“Msaada huu ni mkubwa, chochote ambacho kinapatikana kinafaa kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri wapo wananchi ambao wanachangia elfu moja, na huo ndio utanzania. Tunaendelea kuwashukuru ambao hata hawako hapa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika jambo hili”. Alisema Dkt. Yonazi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages