Wanafunzi wa Shule ya Msingi Changa, wakijibu maswali ya kuhesabu na kusoma wakati wa tamsha la KKK, lililofanyika shuleni hapo leo 8 Novemba 2024
....
Shule ya msingi Changa, iliyoko manispaa ya jiji la Tanga, leo tarehe 8 Novemba 2024 imefanya tamasha la kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi 140 wa darasa la awali, la kwanza na la pili ili kuhamasisha na kukuza stadi za KKK kwa wanafunzi hao.
Mkuu wa Shule hiyo, Bi Stella John Lymo, ameeleza kuwa, tamasha hilo limedhamiria kutoa motisha kwa wanafunzi wa madarasa hayo kupenda kusoma, kuandika na kuhesabu.
“ Dhamira yetu kuu ni kutokuwa na watoto wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika, hivyo tumeona tufanye tamasha hili ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wenyewe, wazazi pamoja na wadau wa elimu tuungane kwa pamoja kufanikisha suala hili”, alisema.
Mwalimu wa darasa la awali wa shule ya Changa, Batuli Msuya, ameeleza kuwa changamoto ya wanafunzi kutokua KKK ilikuwepo shuleni hapo lakini kwa sasa imepata muarubaini kwani shule imeweka mazingira mazuri ya kujifunzia jambo linalowafanya wanafunzi wa madarasa ya chini kupenda kuhudhuria shule na kujifunza kwa bidii.
“Tumefanikiwa katika mkakati wetu wa KKK, na tumepiga hatua kubwa, kutoka kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma kabisa hadi kuwa vianra wa kusoma, kuandika na kuhesabu, jambo linalotupa ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, tunawaomba wadau wa elimu watusaidie kuborasha mazingira ya kujifunzia ili tufanye vizuri zaidi”, alieleza.
Shule ya msingi Chang’a ni moja ya shule kongwe nchini iliyoanzishwa mwaka 1953, ina jumla ya walimu nane, wote wanawake na jumla ya wanafunzi 492 wa darasa la awali hadi la sita.
Mkuu wa Shule ya Msingi Changa, jijini Tanga Bi.Stella John Lyimo, akizunguma na wanafunzi na wageni mbalimbali waliohudhuria tamasha la KKK lililofanyika shuleni hapo leo 8 Novemba 2024
Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Changa, Batuli Msuya, akitoa maelekezo kwa wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na pili katika shindano la kuandika wakati wa tamasha la KKK lililofanyika shuleni hapo leo Novemba 8, 2024
Mgeni rasmi, Diwani wa viti maalum, Bi Mwanaid Kombo akizungumza wakati wa tamasha la KKK lilioandaliwa na Shule ya Msingi Changa, leo Novemba 8, 2024
Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Tanga, Athuamani Baruan akizungumza wakati wa tamasha la KKK lilifanyika shule ya msingi Changa, jijini Tanga, leo 8 Novemba 2024
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Changa, wakijibu maswali ya kuhesabu na kusoma wakati wa tamsha la KKK, lililofanyika shuleni hapo leo 8 Novemba 2024
Wadau mbalimbali wakifuatilia kongamno la KKK katika shule ya msingi Changa, leo 8 Novemba 2024