Breaking

Monday 4 November 2024

SHUWASA YASAINI MKATABA NA GOPA INFRA KUWEZESHA KUBORESHA HUDUMA


Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner wakisaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner wakionesha Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA  baada ya kutia saini.

Na Kadama Malunde- Malunde 1 blog

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imetia saini Mkataba wa Kuijengea Uwezo, baina yake na Mhandisi Mshauri Kampuni ya Gopa Infra ya nchini Ujerumani ikishirikiana na Kampuni ya Superlit Consulting Ltd ya nchini Tanzania.

Mkataba huu wenye thamani ya shilingi bilioni 9 utalenga kuijengea uwezo SHUWASA na wafanyakazi wake ili kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira.

Mkataba huo umesainiwa katika ukumbi wa SHUWASA leo, Jumatatu, Novemba 4, 2024 kati ya Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner.

Akizungumza mara baada ya kusaini Mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, ameeleza kuwa mkataba huo ni wa miaka minne ikiwa ni sehemu mojawapo ya utelekezaji mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya Euro Milioni 76.

“Mhandisi Mshauri huyu atakwenda kutekeleza sehemu mojawapo ya mradi mkubwa wa AFD ambayo ni kuijengea uwezo taasisi, kwanza kufahamu ni maeneo gani yanayohitaji kujengewa uwezo kwa taasisi, watumishi na sehemu zingine katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira,” amesema Mhandisi Katopola.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner wakipongezana baada ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA 

Mhandisi Katopola ameongeza kuwa Mhandisi Mshauri huyo pia ataisaidia SHUWASA katika kusimamia sehemu zingine za utekelezaji wa mradi wa AFD.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na kampuni ya GOPA Infra na Superlit Consulting Ltd katika kuhakikisha malengo ya serikali yanatimizwa hasa katika kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo ya mjini na asilimia 85 katika vijiji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner, ameonesha kufurahishwa baada ya kupata fursa ya kufanya kazi nchini Tanzania na kuahidi kusaidia kuijengea uwezo SHUWASA katika kuhakikisha inatoa wa huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira.
Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner 

“Mtaji wa watu wenye ujuzi na maarifa ni muhimu katika utekelezaji wa mradi huu. Ni muhimu kuwajengea uwezo wafanyakazi wa SHUWASA na Menejimenti kwa ujumla,” amesema Doerner.

Ameongeza kuwa kampuni yake ina uzoefu mkubwa katika kutekeleza miradi mbalimbali duniani.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Superlit Consulting Ltd, Mhandisi Fortunatus Kasimbi, amethibitisha ushirikiano wao na GOPA Infra katika mkataba huo, ukilenga kuwajengea uwezo SHUWASA kwa ujumla.

Amesema watashirikiana kwa karibu kuhakikisha shughuli zinaenda vizuri, kwa ufasaha na ubora unaotakiwa.

“Tutaangalia mifumo iliyopo na kuimarisha ili SHUWASA iweze kujitegemea katika kutekeleza shughuli zake katika kiwango cha kimataifa,” ameongeza Mhandisi Kasimbi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Superlit Consulting Ltd, Mhandisi Fortunatus Kasimbi akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA

Itakumbukwa kuwa mnamo Juni 6 2022 Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), zilitia Saini Mkataba wa Ufadhili wa mkopo wa riba nafuu kwaajili ya mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga ambao unahusisha kuijengea uwezo taasisi, ujenzi wa mtandao wa majisafi kilomita 287 ukarabati wa mtandao chakavu wa majisafi kilomita 100 na ujenzi wa matangi mawili (Kolandoto-lita 1,500,000 na Didia- lita 250,000).

Aidha, mradi huo unahusisha pia ujenzi wa mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi-miwili katika Manispaa ya Shinyanga (Mwagala na Ihapa) na miwili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Kituli na Iselamagazi).

Pia unahusisha ukarabati mkubwa wa mtambo wa kutibu maji Ning’hwa na kufanya tathmini ya ufanisi wa Bwawa la Ning’hwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner wakisaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA leo Jumatatu Novemba 4,2024 - Picha na Kadama Malunde
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto) na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner wakipongezana baada ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA 
Picha ya pamoja baada ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA 
Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner akizungumza baada ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza baada ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza wakati wa kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza wakati wa kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra, Stefan Doerner akizungumza wakati wa kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA
Mshauri Mkuu wa Mshauri wa Kampuni ya GOPA Infra, Dirk Schiemenz akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Mkataba wa Kuijengea Uwezo SHUWASA - Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages