Breaking

Thursday, 7 November 2024

RAIS SAMIA APELEKA NEEMA TABORA

-Aidhinisha Bilioni 19 kusambaza umeme vitongojini

-Kaya 5,940 kutoka katika Vitongoji 180 kunufaika

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 19 wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 utakaonufaisha Kaya 5,940 Mkoani Tabora

Hayo yameelezwa na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle Novemba 07, 2024 Mkoani Tabora mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Paul Chacha wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya Sinotec Company Ltd kutoka nchini China.

“Napenda kuwafahamisha wananchi wa Tabora kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta. Samia Suluhu Hassan ameridhia kiasi cha shilingi 19,057,015,682.55 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 180 mkoani hapa na leo hii tupo hapa kumtambulisha mkandarasi anayetekeleza mradi huu,” alibainisha Mhandisi Dulle.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha alimuelekeza Mkandarasi kuhakikisha anakamalisha kazi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na aliipongeza REA kwa kuendelea kutimiza dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.

Akielezea utekelezaji wa mradi, Mhandisi Dulle amesema unatekelezwa ndani ya majimbo yote 12 ya mkoani humo na kwamba unatekelezwa kwa muda wa miaka miwili na utakamilika Mwezi Agosti, 2026 ambapo kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.

Amefafanua kuwa hadi sasa vitongoji vilivyosambaziwa umeme ni vitongoji 1,323 kati ya vitongoji 3,749 na kwamba vitongoji vitakavyosalia vitasambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mhandisi Dulle amesema Mradi umelenga kusogeza miundombinu ya umeme kwa wananchi katika majimbo yote ili waweze kunufaika na nishati ya umeme katika kujiletea maendeleo hasa katika kuongeza thamani ya mazao, ufundi seremala, viwanda vidogo vidogo, mashine za kusaga na kukoboa sambamba na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

“Vitongoji vitakavyonufaika ni kutoka katika Majimbo ya Sikonge, Urambo, Igalula, Tabora Kaskazini, kaliua, Ulyankulu, Bukene, Nzega Vijijini, Nzega Mjini, Igunga, Tabora Mjini na Manonga ambapo kila jimbo litapata vitongoji 15, Mashine umba 15 na wateja 495 na msongo mdogo (LV) umbali wa kilomita 30,” amefafanua Mhandisi Dulle.

Amesisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wananchi ndani ya vitongoji hivyo ni shilingi 27,000 na kwamba mradi hautakuwa na fidia.

Mhandisi Dulle amesisitiza kuwa Wakala kwa kushirikiana na TANESCO unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyo dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Sinotec Company Ltd, Mhandisi Alphred Kessy alimuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watakamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages