Breaking

Tuesday, 26 November 2024

PROF. KABUDI: UKATILI UNAPASWA KUPINGWA KWA NGUVU ZOTE

  

WAZIRI  wa Sheria na Katiba  Profesa Kabudi  Palamagamba amezindua   rasmi siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia wenye kauli mbiu ya kuelekea miaka 30 ya Beijing chagua kutokomeza Ukatili wa kijinsia.

Akizindua uzinduzi huo leo jijini Dar es Salaam ambapo  wadau na wanaharakati mbalimbali wameweza kushiriki uzinduzi huo,Prof. Palamagamba  amesema ukatili wa kijinsia unapaswa kupingwa kwa nguvu zote.

Amesema suala la  ukatili wa kijinsia ni suala la aibu linalobeza kundi kubwa katika jamii na si la kifahari kulitetea.

''Suala hilo la ukatili wa kijinsia ni suala baya na linalohitaji kutokomezwa na hali budi kuchukuliwa hatua stahiki.

''Katika sheria zetu mbalimbali tunasheria nyingi zinazopinga ukatili wa kijinsia na zinaelezea masuala hayo na kutoa adhabu kali ikiwemo sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 mkiisoma sheria hiyo imeelezea ukatili katika maeneo mengi,''amesema na kuongeza

''Miongoni mwa sheria hiyo imeeleza ukatili wa kutowanunulia nguo watoto wao,kutonunua Chakula kwa watoto ni kosa la jinai  na lipo ndani ya adhabu,usipowatunza watoto lakini pia sheria ya huduma ya msaada wa sheria sura ya 21 nayo inazungumza utoaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto".

Amesema licha ya Tanzania kupiga hatua katika mapambano hayo bado inahitaji kupiga hatua zaidi na kutaka kila mmoja awe balozi wa kupinga ukatili wa kijinsia.

Prof. Kabudi alisema ni adhima ya taifa kuungana katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo vinagharimu maisha ya watu wengi.
''Sasa ni wakati wa kila mmoja wetu kuwa balozi wa kuhakikisha anapinga ukatili wa kijinsia kwani kunasheria mbalimbali zinatambua masuala hayo ya ukatili wa kijinsia",amesema.

Aidha amesema moja ya mambo ambayo hayapaswi kuyaacha  ni kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ''Niwaombe kampeni hii iwe endelevu isiishie kwenye hizi iku 16 ,Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia na utu wa wanawake,''amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa  Bodi Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dk. Monica Muhoja amesema kuna haja ya kuongeza kasi zaidi katika kumuinua mwanamke sambamba na kutungwa kwa sheria maalum za kupinga ukatili wa kijinsia.

 Amesema wanawake na watoto wameendelea kuwa waathirika wa vitendo hivyo na kwamba wako tayari kubainisha mapungufu yaliyopo kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa kuwa walifanya utafiti.

Amesema serikali imekuwa ikishughuļikia maombi mbalimbali wanayowasilisha hivyo kwa mwaka huu wameomba serikali kuendelea kuyachukulia hatua maombi wanayoyaomba kushughulikiwa.

"Mwaka huu tumekuja na maombi mengine ambapo tunaomba Serikali kuweza kuyashughulia ikiwemo ombi la  kutumia juhudi za kuwafikishia kwenye agenda za kiusalama kwa kuhakikisha kuwa masuala ya ukatili wa kijinsia yanaingizwa rasmi katika mipango na mikakati ya kiusalama ya kitaifa .

"Maombi mengine ni pamoja na  serikali ni kuomba kutungwa kwa sheria mahsusi ambayo italinda jamii hasa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia",ameongeza.
Naye Mkurugenzi wa WiLDAF (Women in Law and Development in Africa),Anna Kulaya alisema dhamira ya Kampeni hiyo  ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia huku ikikuza usawa,heshima na haki kwa wote.

“Leo ni siku muhimu sana kwetu sote tunapoanza safari ya kuelekea Siku 16 za Uanaharakati wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Hii ni fursa ya kipekee ya kushirikiana, kuhamasisha, na kuchukua hatua za pamoja dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia kwa ajili ya jamii yenye usawa, heshima, na haki kwa wote.

 “Muungano huu ulipoanzishwa ulikuwa na mashirika tisa tu, lakini kwa miaka kadhaa umeendelea kukua na kuvutia wanachama wengi, kutokana na juhudi zake za pamoja za kupinga ukatili wa kijinsia na kukuza usawa wa kijinsia katika jamii,"amesema. 

Amesema Mkuki ni harakati inayolenga kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kukuza uelewa na kubadili fikra potofu zinazoendeleza ukatili wa kijinsia. 

“Mkuki ni muungano mkubwa wa mashirika zaidi ya 200, unaofanya kazi chini ya uratibu wa WiLDAF (Women in Law and Development in Africa),dhamira yake kuu ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia, huku ikikuza usawa, heshima, na haki kwa wote”, amesema na kuongeza.

 "Kupitia elimu, kampeni za kijamii, na ushirikiano na wadau mbalimbali, Mkuki inalenga kuwa sauti ya mabadiliko na chachu ya jamii yenye amani, heshima, na utu kwa kila mtu bila kujali jinsia,"amesema.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages