Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimehimizwa kuunganisha nguvu na Vyuo Vikuu Huria vilivyopo katika nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuhakikisha kinatoa mchango katika kufanikisha ajenda ya jumuiya hiyo ya kuifanya kuwa kinara wa demokrasia na diplomasia.
Wito huu umetolewa na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda akifungua mdahalo maalamu wa kuenzi mchango wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kuangazia ndoto na maono yake katika kipindi cha miaka 30 ya chuo hiki. Mdahalo huo ukiwa na mada “Miaka 30 ya Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania: Ndoto ya Mwalimu Nyerere Imetimia?”.
“Ni vizuri chuo chetu kikashirikiana na Vyuo Vikuu Huria katika nchi ambazo ni wanachama wa SADC tuone hivi vyuo na dira yake katika kukuza mambo mbalimbali hasa ya demokrasia ili tutoe mchango wetu katika kanda hiyo na namna inavyoweza kutusaidia kuboresha amani, demokrasia na diplomasia” amesema Mhe. Pinda.
Ameongeza kwa kukipongeza chuo kwa kuzalisha bunifu mbalimbali na kutaka vitengo husika kujadili namna ya kupanua wigo wa huduma zake ili kuwafikia wajasiriamali wadogo wadogo mtaani kwa kuwasaidia kufanya tafiti za bidhaa zao wanazozalisha ili zifikie viwango vinavyohitajika na hivyo kuongeza uzalishaji wa bidhaa zetu nchini.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof Elifas Tozo Bisanda, amesema lengo la kuandaa siku hii maalumu ya kumbukumbu ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania ni kutoa heshima kwa hayati baba wa taifa ambaye tunamuhesabu kama ndiye muasisi wa kuanzishwa kwa chuo hiki.
“Katika utoaji wa elimu masafa na huria kwa miaka 30 tumeweza kukipeleka chuo mbele huku tukitimiza ndoto ya Mwl. Nyerere kwani mwanafunzi anaweza kusoma mahali popote kwa wakati wowote, tumewekeza vyema kwa kuweza kuendelea kutoa elimu huria kwa ufanisi zaidi, hii yote ni kwa sababu ya msaada na uwezeshaji wa serikali." Amesisitiza Prof. Bisanda.
Pia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku ameelezea mchango wa Mwl. Nyerere katika chuo hiki kwa kutaja moja ya ndoto ya mwalimu ilikuwa kuwezesha utoaji elimu wa kumfikia kila Mtanzania akiangalia usawa na heshima kwa kila binadamu. Elimu ambayo ingeongeza uwezo wa wananchi akidhamiria kuongeza maarifa ya kufikirika kwa jamii, hivyo tukiangazia elimu inayomfikia kila mtu ndipo tunaona maono ya Baba wa Taifa yamepiga hatua kwa OUT kwa kuweza kufikia wengi kupitia elimu huria ,masafa na mtandao.
Naye Makamu Mkuu wa Kwanza wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Geoffrey Mmari amekipongeza chuo hiki kwa kuendelea kutoa elimu huria, masafa na mtandao kwa ufanisi huku kikizidi kuboresha miundombinu ya teknolojia za ufundishaji na ujifunzaji sambamba na kuendelea kutimiza ndoto ya Mwalimu kupitia utoaji wake wa elimu huria.