Breaking

Friday, 1 November 2024

MISHENI ZA UANGALIZI UCHAGUZI MKUU BOTSWANA ZATOA TAARIFA ZA AWALI KUHUSU UCHAGUZI HUO ULIVYOENDESHWA

Misheni za Uangalizi uchaguzi mkuu wa Botswana kutoka Jumumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC-SEOM), Umoja wa Afrika (AU_EOM) na Jukwaa la Tume za Uchaguzi la SADC (ECF) zimetoa taarifa za awali kuhusiana na uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 30 Oktoba 2024.

Akıwasilisha taarifa hiyo jijini Gaborone,kwa upande wake Mkuu wa Misheni ya SADC-SEOM Mhe.Mizengo Pinda amesema katika uchaguzi huo SEOM imeona kuwa mazingira ya kisiasa nchini humo yalikuwa ya utulivu na yenye amani kuanzia kipindi cha kampeni , siku ya kupiga kura na hata baada ya kupiga kura.

“SEOM iliona kuwa shughuli za kisiasa kuanzia hatua za awali kuelekea siku ya uchaguzi na siku ya kupiga katika Jamhuri ya Botswana zilifanyika kwa amani na kwa utulivu mkubwa na hivyo kuwawezesha wananchi wa Botswana kutumia haki yao ya kimsingi ya kidemokrasia ya kupiga kura, kwa utulivu na amani pia,” alisisitiza Mhe. Pinda.

Ameongeza kuwa SEOM ilishuhudia vyama vya siasa na wagombea binafsi nchini humo wakiendesha kampeni kwa uhuru na amani ambazo zilifanyika kupitia mikutano, nyumba kwa nyumba, midahalo kwa wagombea wa urais , mahojiano na mijadala katika vyombo vya Habari na mabango katika sehemu mbalimbali nchini humo ambapo amesema katika shughuli zote hizo hakukuwa na vurugu wala fujo hali iliyoonesha uvumilivu wa hali ya juu wa kisiasa na ukomavu kwa watu wa Botswana.

Akiongelea zoezi la upigaji kura la awali lililofanyika tarehe 19 na 26 Oktoba 2024, Mhe.Pinda alisema kuwa zoezi hilo liliendeshwa kwa amani licha ya kuwepo kwa tukio la mpiga kura mmoja kuondoka na karatasi ya kupigia kura na baadhi ya vyama kulalamika kuondolewa kwa mabango yao na kuongeza kuwa askari polisi walikuwepo katika mikutano ya kampeni katika maeneo yote na kuliendelea kuwa na amani hata pale ambapo hakukuwa na askari polisi.

Amesema SEOM iliangalia masuala mbalimbali ya muhimu kabla na wakati wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na hali ya siasa na usalama chini humo, usimamizi wa uchaguzi, ripoti za vyombo vya habari kuhusu uchaguzi, na uwakilishi wa jinsia na Makundi maalum ambayo yote yametekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Akiwasilisha taarifa ya misheni yake Mkuu wa Misheni ya AU_EOM na Rais wa zamani wa Nigeria Mhe. Goodluck Jonathan amesema AU pia inawapongeza wananchi wa Botswana kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na uvumilivu wa hali ya juu katika kipindi chote cha uchaguzi, na kuwasihi kuendelea hivyo kwakuwa siasa si uadui bali ni ushindani wa hoja na kupigiana kura zitakazoamua kupitia uchaguzi.

Naye Mkuu wa misheni ya SADC _ECF na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania Mhe. Jaji Jacob Mwambegele ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini humo kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu wakati mamlaka za usimamizi wa uchaguzi zikikamilisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi, akiwaomba kuendelea kuhamasisha amani, uvumilivu, na utulivu kupitia majukwaa mbalimbali katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi.

Kulingana na Misingi na Miongozo ya SADC inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia iliyorekebishwa mwaka 2021, misheni hizo za SADC na AU zitatoa taarifa ya mwisho kuhusu uchaguzi siku 30 baada ya kutoa taarifa ya awali ambayo itawasilishwa kwa Serikali ya nchi hiyo ili kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa hizo na hivyo kuboresha mazingira ya ufanyaji uchaguzi mkuu mwingine ujao nchini humo.

SEOM ilipeleka waangalizi 72 waliotoka katika nchi 10 wanachama wa SADC ambao walikwenda katika wilaya 9 za kiutawala za nchini humo za Kati, Ghanzi; Kgalagadi; Kgatleng; Kweneng; Ngamiland; Kaskazini Mashariki; Kusini na Kusini Mashariki.

Siku ya Uchaguzi tarehe 30 Oktoba, 2024 Misheni hizo zilitembelea vituo vya uchaguzi kuangalia namna zoezi linavyoendeshwa na pia zilishuhudia awamu ya pili ya upigaji kura wa awali uliofanyika tarehe 26 Oktoba,2024.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages