Breaking

Thursday, 14 November 2024

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA VIWANDA VYA ELSEWEDY ELECTRICITY NA KNAUF KWA UTEKELEZAJI WA SHERIA ZA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, akiwa na Mkurugenzi mtendaji wa Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar wa kiwanda cha Elsewedy Electric, kilichopo Kigamboni kibada jijini Dar es salaam, katika ziara aliyoambatana na Kamati ya kudumu ya Bunge na Ustawi na maendeleo ya jamii wakiwa na mwenyeji wao OSHA iliyofanyika tarehe 12 novemba 2024.

*********************

Mwandishi wetu Dar es salaam

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii yapongeza Viwanda vya Elsewedy Electricity na Knauf kwa Utekelezaji wa Sheria za Usalama na Afya Mahali pa Kazi

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeeleza kuridhishwa kwake na hali ya usalama na afya mahali pa kazi katika kiwanda cha kutengeneza Nyaya za umeme na Transfoma cha Elsewedy Electric Kigamboni Jijini Dar es salaam na Kiwanda cha kutengeza gypsum cha Knauf Mkuranga Mkoani Pwani. Pongezi hizo zimetolewa baada ya ziara ya kamati hiyo katika ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na viwanda hivyo, iliyofanyika Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam na Pwani.

Ziara hiyo iliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda. Wajumbe wa kamati hiyo walitembelea maeneo ya kazi na kujionea utekelezaji wa sheria za usalama na afya mahali pa kazi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatma Toufiq, alitoa pongezi mara baada ya kutembelea viwanda hivyo, amesema Viwanda hivyo vimekuwa mfano mzuri kwa kufuata sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi, akisema kamati hiyo itaendelea kutoa ushauri kwa serikali kuhusu umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya wafanyakazi

“Tuko na wenzetu wa OSHA ambao ni miongoni mwa taasisi ambazo zipo chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii ambapo tumetembelea maeneo mbalimbali kuangalia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahali pa kazi

Kwa taarifa tulizopata awali Knauf ni miongoni mwa kampuni ambazo zinafuata sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi vizuri na tumekuja kujionea wenyewe, Sisi kama kamati tumekuwa tukiishauri serikali jinsi gani suala la usalama na afya mahali pa kazi linatakiwa liwe ili kulinda ustawi wa wafanyakazi pindi wanapo kuwa kazini na tutaendelea kuishauri ”alisema Mhe. Toufiq.

Awali akizungumza mara baada ya ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ambao wanazalisha na kusafirisha bidhaa nje ya nchi, hali inayo changia kukuza uchumi wa Taifa Pamoja na kutoa fursa kwa vijana kupata ajira katika viwanda hivyo.

Sambamba na hayo, Mhe. Ridhiwani aliupongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara amabazo zimepelekea viwanda hivyo kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Nitumie nafasi hii kuupongeza uongozi wa OSHA chini ya Mtendaji Mkuu Bi. Khadija Mwenda kwenye viwanda vyote tulipo fika kabla ya kuanza kutembelea kiwanda lazima muingie kwenye chumba maalumu kupata maelekezo ya usalama na afya hususani kuhusu mambo mtakayo kutana nayo lakini pia namna ya kuweza kujilinda “ alisema Mhe Ridhiwan

Amesema amefurahishwa namna ambavyo mifumo iliyowekwa Viwandani hapo vinavyofanya kazi na jinsi vinavyoweza kumlinda mfanyakazi

“Nilicho kipenda zaidi ni namna ambavyo mifumo inavyofanya kazi Viwandani hapo ukisogelea au kugusa uzio wa mashine, mitambo inazimika yenyewe jambo ambalo ni hatua kubwa sana katika kulinda usalama wa wafanya kazi, na haya yote ni matokeo ya kaguzi zinazo fanywa na OSHA mara kwa mara imepekea kufikia hatua nzuri za kiusalama maeneo hayo hali hii ni ishara nzuri ya kazi bora inayo fanywa na wenzetu wa OSHA pia ni ishara nzuri kwa Mtendaji mkuu kuendelea kusimamia maagizo ya mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan, sisi wasaidizi wa mheshimiwa Rais kazi yetu nikuleta ujumbe na kuhakikisha watanzania wanakua salama kama anavyotaka Rais, Kwa hakika naridhishwa sana na kazi ambayo OSHA mnaifanya “alisema Mhe. Ridhiwani.

Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi Bi.Khadija Mwenda, amewasisitiza Waajiri nchini kuendelea kuzingatia sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Bi.Mwenda, amesema maeneo ya kazi yanapozingatia usalama na afya kunaongeza uzalishaji kutokana na kupunguza vihatarishi kwenye maeneo yao na hivyo kuongeza uzalishaji.

“leo tulikuwa na Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendelo ya Jamii ambayo ilikuja kuangalia jinsi ambavyo OSHA inasimamia sheria ya usalama na afya mahali pa kazi, kimsingi huu ni utekelezaji wa maelekezo tuliyo pewa tulipo kutana na Kamati ya Bunge tulitoa taarifa nzuri na kamati wakaridhishwa nayo lakini wakataka kujionea na leo wamekuja wamejionea.

kwenye kiwanda hiki cha Knauf uwekezaji unaongezeka mara dufu kwa sababu ya mazingira na mifumo mizuri iliyopo hivyo nitoe rai kwa wawekezaji na wafanya biashara wawekeze kwenye mifumo ya usalama na afya ili kulinda wafanya kazi.” alisema Bi.Khadija Mwenda.

Naye mwanasheria wa kiwanda cha Knauf, Flora Erasto aliishukuru kamati ya Bunge Pamoja na OSHA kwa kufanya ziara kiwandani hapo huku akieleza kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikifanya kazi kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na OSHA tangu kuanzishwa kwake nah ii ndio imetufanya kuwa bora zaidi.

“kwanza tunaishukuru sana OSHA tangu kuanza kwa kiwanda hiki tumekuwa tukifanya kazi na OSHA vizuri na wamekuwa wakitushauri na kutupa maelekezo muhimu kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi , pia tunaishukuru serikali kwa kutoa miongozo mizuri na nafasi nzuri ambayo imekuwa ikitusaidia sisi kama wawekezaji.”alisema Frola.

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni taasisi iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu wenye jukumu la kusimamia masuala ya usalama na Afya mahali pa Kazi.

Mwakilishi wa usalama na afya mahali pa kazi kutoka katika kiwanda cha Knauf kilichopo Mkulanga akitoa maelezo juu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete na Kamati ya kudumu ya Bunge na Ustawi na maendeleo ya jamii, wakiwa na wenyeji wao OSHA katika ziara ya siku moja iliyofanyika tarehe 12 novemba 2024.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa Kamati ya kudumu ya Bunge na Ustawi na maendeleo ya jamii wakiambatana na wenyeji wao OSHA, wakipewa ufafanuzi juu ya maswala ya usalama na afya na msimamizi wa masuala ya usalama na afya  katika kiwanda cha Elsewedy Electric kinachojihusisha na utengenezji wa vifaa vya umeme, Bwana Hashim Kanjoka,kilichopo Kigamboni Kibada, jijini Dar es salaam.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge na Ustawi na maendeleo ya jamii akiuliza swali kwa Mkurugenzi mtendaji wa Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar i wa kiwanda cha Elsewedy Electric, kilichopo kigamboni, kibada jijini Dar es salaam katika ziara ya siku moja iliyofanyika tarehe 12 novemba 2024.

Msimamizi wa masuala ya usalma na afya mahali pa kazi, Bwana Hashim Kanjoka akitoa maelekezo na historia fupi ya kiwanda cha kuzalisha vifaa vya umeme cha Elsewedy Electric kilichopo Kigamboni Kibada, jijini Dar es salaam kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete,alieambatana na kamati ya kudumu ya Bunge na Ustawi na maendeleo ya jamii, Pamoja na wenyeji wao OSHA, kabla ya kuanza ukaguzi wa maswala ya usalama na afya katika kiwanda hicho.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages