Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo (aliyesimama) akizungumza na Wadau wa Kemikali Bashirifu katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Jengo la Ushirika Novemba 13, 2024. Kushoto ni Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa na kulia ni Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ziliwa Machibya.
***********************
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imewataka wauzaji wakubwa wa kemikali kuacha kuwauzia wauzaji wa kati na wadogo wa kemikali ambao hawajasajiliwa kufanya biashara hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, wakati wa kikao na wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa kemikali bashirifu kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika katika Ofisi za Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam.
“Wadau wote wa kemikali lazima wawe wamesajiliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa sheria pamoja na kutimiza maazimio tulioweka ili waweze kufanya biashara zao kwa usalama ili kulinda afya za binadamu na mazingira,” alisema Mkurugenzi Ndiyo.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ziliwa Machibya, amesema kuwa kemikali bashirifu ni hatari katika mazingira ya matumizi ya dawa za kulevya hivyo, amewasihi wadau wa kemikali bashirifu kufuata taratibu za usajili ili ziweze kutumika katika matumizi yaliyokusudiwa katika uzalishaji mbalimbali na kwa usalama.
Kwa upande wake Geoffrey Jato ambaye ni mdau wa kemikali ameipongeza Mamlaka kwa kuwapa elimu na kuendelea kuweka ushirikiano wa karibu na wadau wa kemikali jambo ambalo limeweza kuwatatulia changamoto mbalimbali zikiwemo usajili.
“Elimu tuliyoipata ya usajili wadau wengi hawakua nayo, ila kwa sasa wingi utaongezeka wa wadau kujisajili na kupata elimu ili wanapofanya manunuzi ya kemikali au uzalishaji waweze kufanya kwa usalama,” alisema Jato.
Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa (aliyesimama), akiwasilisha mada kuhusu Udhibiti wa Kemikali Bashirifu katika Mazingira ya sasa.
Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai kutoka, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ziliwa Machibya (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu ushiriki wa Sekta Binafsi katika kudhibiti kemikali bashirifu.
Washiriki wa Kikao cha Wadau wa Kemikali Bashirifu wakiuliza maswali pamoja na kutoa mapendekezo katika kikao hicho.
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wadau wa Kemikali Bashirifu wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 13, 2024.
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo (katikati) akiwa na Viongozi pamoja na Wadau wa Kemikali Bashirifu mara baada ya kikao na wadau hao kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 13, 2024.