Breaking

Sunday, 3 November 2024

DAWASA YABAINISHA MAFANIKIO UTOAJI HUDUMA MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA

 


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana ya uboreshaji wa huduma ya majisafi kwa Mkoa wa Dar es Salaam hususani katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa katika Jiji la Dar es Salaam, Mamlaka imefanikiwa kusambaza huduma ya maji kwa asilimia zaidi ya 93 ambapo nje ya mahitaji ya maji ya wananchi ya lita milioni 685, Mamlaka mpaka sasa imeweza kutoa lita milioni 534 za maji kwa siku sawa na asilimia 93.

Ameongea pia kuwa katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa kipindi chote cha mwaka, Serikali kwa kushirikiana na DAWASA inatekeleza mradi mkubwa wa kuhifadhi maji wa Bwawa la Kidunda utakaokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita Bilioni 190.

Ameeleza kuwa Mamlaka imeendelea na jitihada za uzalishaji wa maji kutoka kwenye vyanzo vya juu ya ardhi ikiwemo ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji Mshikamano wenye tenki la lita milioni 6, mradi wa kusambaza maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo unaonufaisha wakazi 450,000, mradi wa maji Dar es Salaam ya Kusini unaotarajia kunufaisha 450,000 wa Kinyerezi, Segerea, Tabata, Ubungo na Ilala.

Pia kwa vyanzo vya maji ya chini ya ardhi Mamlaka imetekeleza mradi wa visima 7 vya Kigamboni vinavyozalisha lita milioni 20, na mpango uliopo ni kuongeza uzalishaji wa maji ya visima kwa kuweka pampu ili kukuza uzalishaji kufikia lita milioni 44 kwa siku.

Mhandisi Bwire amebainisha pia kuwa kwa sasa Mamlaka ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 198 ambalo ni ongezeko kutoka lita milioni 158 za awali. Na ongezeko hili la maji limepatikana kupitia kwenye matenki ya maji ya Bangulo la lita milioni 9, Tegeta A la lita milioni 5, Mbweni milioni 5, na tenki la maji Mshikamano la tenki la lita milioni 6.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Kigamboni Mhe. Ernest Mafimbo amesema kuwa hali ya maji kwa Kigamboni ni nzuri na imefika asilimia 55 ambapo kuna wakazi 331,000.

Awali hali ya maji ilikuwa ngumu sana maana wengi walikuwa wanatumia maji ya visima ambavyo havikuwa na tija sana, lakini baada ya mradi wa DAWASA wa visima virefu hali ya majisafi imeimarika sana hususani kwenye Kata yaa Kibada, Mjimwema na kufika Kata ya Somangila.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages