Na Mwandishi Wetu - Malunde 1 blog
Benki ya CRDB tawi la Nzega Mjini imekabidhi Viti 40 pamoja na viti 40 kwenye shule ya sekondari Itobo iliyopo Wilayani Nzega Mkoani Tabora.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika leo Novemba 04, 2024 katika shule ya sekondari Itobo ambapo CRDB benki imekabidhi viti pamoja na meza hizo ikiwa ni sehemu ya gawio la asilimia 1 inayorudishwa kwenye jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi meza na viti, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana amesema benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kuisaidia jamii kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya na elimu ikiwa ni kuiunga mkono serikali na kuisaidia jamii kupitia gawio hilo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya makabidhiano Kaimu mkuu wa wilaya ya Nzega ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Uyui Mohamed Mtuliakwako ameipongeza benki ya CRDB kwa kutoa viti na meza hizo na kutoa rai kwa wanafunzi na walimu kuzingatia utunzaji wa meza na madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa na manufaa kwa wanafunzi.
"Serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha na kuweka mazingira mazuri katika sekta ya elimu, kama ujenzi wa madarasa, lakini pia tunaendelea kuwapongeza wadau wetu wa benki ya CRDB kwa kuendelea kuiunga mkono serikali yetu kwenye sekta mbalimbali hapa nchini ambapo tunaona leo hii tumekabidhiwa madawati 40 yatakayokwenda kupunguza adha ya ukosefu wa viti na meza kwa wanafunzi", amesema.
"Waswahili wanasema kitu kitunze kikutunze hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu hapa shuleni kulinda viti na madawati haya ili yaweze kutusaidia na kuvisaidia vizazi na vizazi kwenye shule yetu ya Itobo, tusipovitunza azima ya benki ya CRDB itakuwa haijatimia lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu kwenye mazingira mazuri", ameongeza Mtuliakwako.
Akisoma taarifa fupi ya shule hiyo Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya Nzega ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari Dkt. Christopher Semnyamanza amesema kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa meza na viti kwa wanafunzi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyopo.
"Shule ya sekondari Itobo ina jumla ya wanafunzi 525 kati ya wavulana wakiwa ni 211 na wasichana 314 huku madawati yakiwa ni 411 kwa shule nzima ujio wa CRDB imekuwa ni mkombozi kwa wanafunzi kwani meza na viti hivyo vitapunguza changamoto ya kukaa wawili wawili kwenye meza moja, tunayo furaha kubwa kwa kupatiwa madawati haya, tuendelee kuiomba benki ya CRDB iendele kutuunga mkono kwani uhitaji bado ni mkubwa kwenye shule yetu", amesema Dkt. Semnyamanza.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Itobo akiwemo Rosemary Masatu na Omary Hamisi wamesema hapo awali walipitia changamoto ya kukaa chini na wengine kutumia madawati ya shule ya msingi wakati wa kujifunza hali iliyopelekea kushindwa kujifunza vizuri, wanaishukuru benki ya CRDB kwa kutoa msaada huo.
Msaada huo wa Benki ya CRDB ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kusaidia wanafunzi wa shule ya sekondari Itobo kupata elimu bora.
Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya makabidhiano Kaimu mkuu wa wilaya ua Nzega ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Uyui Mohamed Mtuliakwako akizungumza.
Mkuu wa shule ya sekondari Itobo Benson Mwaipungu akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Kaimu mkurugenzi halmashauri ya Nzega ambaye pia ni afisa elimu sekondari Dkt. Christopher Semnyamanza akizungumza kwenye hafla hiyo ya makabidhiano.
Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Nzega Yohana Bunzali akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Itobo akizungumza mara baada ya kukabidhiwa madawati shuleni hapo.