Breaking

Wednesday, 16 October 2024

WIZARA YA MADINI KUREJESHA MINADA YA NDANI NA KIMATAIFA MADINI YA VITO



●Itafanyika ndani ya nchi na nje ya nchi

●Itaendeshwa na Tume ya Madini kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania

●Marekebisho ya Sheria na Kanuni yakamilika

⚫️ Ni utekelezaji wa Rais Samia kukuza biashara ya Tanzanite


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Madini inarudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya uzalishaji hususan Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es salaam, Arusha na Tanga na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini Thailand.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 16, 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amesema kuwa baada ya taratibu za marekebisho ya kisheria kukamilika juu ya uendeshaji wa minada hiyo wanatarajia ndani ya muda mfupi ujao kuanza taraibu za kuweka miundombinu ya kuanza minada ya ndani.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.

Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya Nishati na Madini kuwa, Mpango wa kurejesha minada ya madini ya vito ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha jijini Mwanza tarehe 13 Juni, 2024.

Kwa upande wake , Naibu Waziri wa madini Dkt.Steven Kiruswa amesema, kwa sasa wataalam wa Wizara ya Madini wamepata uzoefu mkubwa katika minada na maonesho ya kimataifa baada ya kujifunza namna biashara za kimataifa zinavyofanyika pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani madini katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani , India , Afrika Kusini na Thailand.

Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu uboreshaji na utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Masoko na vituo, minada ya ndani na kimataifa ya madini ya vito kwa Kamati hiyo, Kaimu Mtendaji Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa, minada hiyo itaendeshwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa la Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa mauzo wa kielektroniki ambapo usimamizi utahusisha shughuli za uthaminishaji na upangaji wa madini ili kuweza kupata bei nzuri kulingana na madini husika,akisisitiza kwamba lengo kuu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na usonara barani Afrika.

Mhandisi Lwamo ameongeza kuwa, minada ya vito itaifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo Utalii na biashara katika kipindi husika ikiwa ni pamoja na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameendelea kumpongeza Waziri wa Madini na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ya kuisongesha Sekta ya Madini katika ngazi ya kimataifa inayoleta tija katika uchumi wa nchi na hasa katika mkakati wa kurudisha hadhi na thamani ya madini ya vito yakiwemo madini ya Tanzanite ambayo ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages