Breaking

Monday, 7 October 2024

TIRDO YAWATAKA WATENGENEZAJI WA MKAA MBADALA KUJITOKEZA KUPATA ELIMU

SHIRIKA la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limetaka watengenezaji wa mkaa mbadala kujitokeza kupata elimu ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi kwani asilimia 50 ya mkaa huo unaotumika katika maeneo mbalimbali hauna ubora kutokana na watengenezaji wake kufanya shughuli hiyo bila kupata mafunzo yakitaalamu.

Kauli hiyo imetolewa leo Octoba 7,2024 na  Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO  Profesa Mkumbukwa  Mtambo wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema takwimu hiyo imetokana na tafiti waliyofanya katika mikoa 12 kwa ajili ya kuwabaini  wanaotumia mkaa mbadala kupitia mradi wa kukuzq matumizi wa nishati hiyo ambapo mkoa wa Dar es Salaam umeonekana  kuongoza kuwa na watumiaji wengi.

“Mradi huu ulianza mwaka 2022,tulianza kuwabaini watengenezaji wa mkaa mbadala katika mikoa 12 ambapo tulikusanya takribani watumiaji 59,katika kuangalia ubora wa mkaa tulikuta sampuli  zaidi ya 43 ambazo ni zaidi asilimia 50 hazina ubora,”amesema Profesa Mtambo.

Amesema kupitia utafiti huo pia wamegundua changamoto za malighafi ya utengenezaji wa mkaa mbadala ambapo imeonekana watengenezaji wengi wanatumia mabaki ya mkaa yanayotokana na kuni ambayo yanatoa mkaa wenye ubora  ambao wanaupiga vita.

“Kutokana na hali hiyo tumetoa mafunzo kwa watengenezaji  zaidi  ya 30 kwenye mikoa 11 tuliyoifanyia utafiti na tunaendelea kuwaita  watengenezaji wengine waje kupata mafunzo Tirdo,”amesema Profesa Mtambo. 

Amesema mbali na hilo utafiti pia umeonyesha wanaopaswa kutumia mkaa mbadala hasa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 ambazo ni 127 zilizofanyiwa utafiti  asilimia 52 bado wanatumia kuni hivyo changamoto bado ipo.

Profesa Mtambo amewakaribisha watengenezaji wa mkaa na watumiaji kufika katika ofisi hiyo kwa ajili ya utengenezaji wa nishati hiyo kupitia mradi hio ambao unaendelea.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA) Dk.Donald Mmari amesema wameshriki  katika mradi huku akisema moja  ya jambo ambalo wamelibaini  katika tafiti  ni uharibifi wa mazingora unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni nchini.

“Mwaka  2015 upotevu wa misitu hekta 372,000 lakini maiaka saba bada yaani ilipofika mwaka  2022 upotevu umefika hekta takribani 400,000 tukaona hiyo ni mbaya sana,watu wanakata miti inaleta madhara ikiwemo hewa ya ukaa lakini pia kuongezeka kwa ukame na majanga,”amesema Dk.Mmari.

Amesema kama taasisi waliona wafanye utafiti ambapo walianza kwakuangalia  kuhusu utumiaji wa mkaa na faida zake kiafya.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages