Breaking

Tuesday 22 October 2024

TEA YAPITIA NA KUTATHMINI MPANGO MKAKATI WAKE WA UTEKELEZAJI.

Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Erasmus Kipesha, imekutana kwa siku mbili kuanzia Oktoba 21 na 22, 2024, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026).

Tathmini hiyo imelenga kubaini maeneo ya kuboresha na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya TEA.

Dkt. Kipesha, akizungumza na wajumbe wa Menejimenti, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha majukumu ya TEA yanaenda sanjari na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kuwa bora, salama, na endelevu katika shule na vyuo.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Menejimenti walipata fursa ya kujadili namna bora ya kusimamia na kutekeleza Mpango Mkakati huo katika kipindi kilichosalia cha miaka miwili, ili kuhakikisha malengo yote ya TEA yanafikiwa kwa ufanisi zaidi.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilianzishwa kupitia Sheria ya Bunge Na. 8 ya mwaka 2001, chini ya kifungu 5 (1), pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013, kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu.

Lengo kuu la Mfuko wa Elimu ni kuimarisha juhudi za serikali katika kugharamia miradi ya elimu ili kuinua ubora na upatikanaji wake kwa usawa, katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania Bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus F. Kipesha akisisitiza jambo katika kikao maalumu cha Menejimenti cha kutathmini Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Mamlaka pamoja na majukumu yake.
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Taasisi CPA Mwanahamis Chambega (Kulia) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Bw. Emmanuel Shirima wakifuatilia wasilisho la tathmini ya Mpango Mkakati wa TEA katika kikao maalumu cha Menejimenti kilichofanyika kwa lengo la kupitia Mpango huo.

Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda akifafanua jambo kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa TEA pamoja na utekelezaji wa majukukumu ya Mamlaka hiyo.
Meneja Ufuatiliaji na Tathmini Bi. Wendo Chiduo (Kulia) na Meneja Rasilimali Watu Bi. Alice Lukindo (Kushoto) wakifuatilia wasilisho la tathmini ya Mpango Mkakati wa TEA katika kikao maalumu cha Menejimenti kilichofanyika kwa lengo la kupitia Mpango huo.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti wakifuatilia wasilisho la tathmini ya Mpango Mkakati wa TEA katika kikao maalumu kilichofanyika kwa lengo la kupitia Mpango huo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages