Breaking

Thursday, 10 October 2024

WAZIRI SILAA- KONGAMANO LA TEHAMA TANZANIA 2024 , AI NA ROBOTI YATAPEWA KIPAUMBELE

*Azungumzia uwekezaji uliofanywa na Serikali katika TEHAMA

*Asema Tanzania Kinara Afrika kwenye Usalama Mtandao

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine duniani katika kukuza uchumi wa kidijitali kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya TEHAMA.

Waziri Silaa aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Jukwaa la Jamii ya Habari Duniani (WSIS) Kanda ya Afrika, kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, tarehe 9-11 Oktoba 2024.

“Rais Samia amezindua mkakati wa Tanzania ya Kidijitali wa miaka 10 (2024-2034) unaoonesha jinsi Tanzania itakavyojumuisha TEHAMA kwenye uchumi na masuala ya kijamii,” alisema Waziri Silaa.

Aliongeza kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na ujenzi wa minara ya mawasiliano, pamoja na kuanzisha sera na sheria mbalimbali zinazolenga kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Waziri Silaa alimtaja Rais Samia kama kiongozi aliyewezesha na kutoa maelekezo yanayowezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na hivyo kupelekea Tanzania kuibuka kidedea katika masuala ya TEHAMA.

Aidha, Waziri Silaa alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha washiriki wa Kikao kazi hicho kushiriki katika Kongamano la Nane la TEHAMA Tanzania la mwaka 2024, litakalofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi atakuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Silaa amebainisha kuwa katika Kongamano hilo masuala ya akili mnemba (AI) na roboti yatapewa kipaumbele, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa kuhusu teknolojia hizo kutokana na mchango wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, Waziri Silaa alisisitiza kuwa Tanzania ni miongoni mwa vinara wa usalama mtandao Duniani na ikiwa moja kati ya nchi 5 kutoka barani Afrika, akitolea mfano Jarida la Kimataifa la kupima ukomavu wa Usalama Mtandao kwa kila nchi (Global Cybersecurity Index) lililotolewa tarehe 23 Septemba, 2024 ambalo hutolewa kila miaka minne (4) na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU).

Alifafanua kuwa ulinzi wa kimtandao unapaswa kuwa kipaumbele, kwani kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na ukuaji wa uchumi wa kidijitali shughuli nyingi, ikiwemo huduma za kifedha na uhifadhi wa taarifa binafsi, zinafanyika mtandaoni.

Kwa kuimarisha usalama wa mtandao, Tanzania ina Sheria nzuri za Usalama Mtandaoni, mikakati mizuri ya Usalama Mtandao na uwepo wa Kitengo cha TZ-CERT kilichopo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambacho kinajihusisha na ulinzi wa mtandao na kubaini mashambulizi kabla hayajatokea kwa ujumla ni baadhi ya masuala yaliyochangia kuifanya Tanzania kuibuka kinara katika Usalama Mtandao Duniani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages