Na Grace Semfuko, Maelezo
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali inatambua umuhimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii, na ndio maana inawekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta hiyo muhimu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Oktoba 17, 2024 Jijini Dar es Salaam, katika kilele cha kongamano la nane la TEHAMA na kuongeza kuwa, serikali imeweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria katika kuhakikisha uwekezaji katika TEHAMA unafanya vizuri nchini.
“Serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa masuala ya TEHAMA katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii na namna inavyofanya jitihada zake katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafidika na uwepo wa matumizi ya TEHAMA, moja ya jitihada hizo ni kujenga mifumo muhimu ya uendeshaji pamoja na mazingira wezeshi ya kisera na sheria” amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amesema wizara yake imeanza maandalizi ya urushaji wa satellite ambapo mpango mkakati wa miaka mitano ya program ya anga za juu umeanza kuandaliwa.
Amesema maandalizi hayo ni pamoja na utungaji wa sera, sheria na kuridhia kwa mikataba ya kimataifa ya masuala ya anga za juu ambapo taasisi ya teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) imepata mradi wa utafiti wa kuwezesha kurusha satellite kupitia mradi unaosimamiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu (UNOOSA) kwa kushirikiana na taasisi ya anga za juu ya Japan
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso amesema taasisi nyingi zilizopo chini ya wizara ya habari zimekuwa na mabadiliko makubwa katika uwekezaji huku akitolea mfano uwekezaji wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano pamoja na anwani za makazi.
“Sisi kama Bunge ni mashuhuda na tumeshuhudia kila taasisi katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na TYeknolojia ya Habari uwekezaji wake mkubwa, kwenye mkongo wa Taifa wa mawasiliano umefanya vizuri, tumeongeza fedha ambazo zimeleta tija, na karibu kila sehemu tumeshuhudia upatikanaji wa huduma ya mkongo wa taifa ambao unafanya kazi mpaka maeneo ya wilayani, tumeona jitihada za serikali ambazo zimefanywa na serikali ya awamu ya sita kuhakikisha wanapeleka huduma za anwani za makazi karibu maeneo yote nchini” amesema Mhe. Kakoso.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema tangu kuanza kwa makongamano hayo mwaka 2017, wamekuwa wakiangalia na kujadili teknolojia mbalimbali ambazo zinaleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ambapo kwa mwaka huu kongamano hilo limeangazia masuala ya akili mnemba na roboti, ili kunagalia ni kwa namna gani hayo mambo yanaleta mabadiliko ya kiuchumi ambapo limepata mwitikio wa wataalamu kutoka katika mataifa mbalimbali Duniani ambao wameshiriki katika kutoa mada.