Breaking

Tuesday, 8 October 2024

NCHIMBI ‘AFUNGA’ OFISI ZA CHADEMA ITILIMA


-Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Itilima, Katibu na wanachama wao wahamia CCM.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, Ndugu Terry Kilugala, na Katibu wake wa Wilaya ya Itilima, Ndugu Gershom Migasa Mipawa, pamoja na wanachama wao zaidi ya 60, wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa na Katibu Mkuu wake, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Luguru, wilayani Itilima.

Ndugu Kilugala, akizungumza kwenye mkutano huo, amesema mbali na Chadema kuwatumia vibaya viongozi na wanachama wake, kisha kuwaacha ‘watupu’ wakiangaliana wenyewe kwa wenyewe, uongozi wa CCM na utendaji kazi wa serikali yake, chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, vyote vimemfanya arudi nyumbani.

“Tulikuwa tunaenda Mwanza siku mbili kwa ubovu wa barabara, leo tunaenda na kurudi. Lazima tuseme ukweli, CCM imefanya kazi, lakini wenzetu wamebakia kusema uongo na kututumia vibaya. Kuna wabunge wa COVID-19, lakini ndani yake wamo wake zao, alafu huku wanatudanganya.”

Balozi Nchimbi, akiwapokea, amesema:

“Hawa ndugu zetu wameona mbali mapema, maana viongozi wakubwa kama Peter Msigwa kaona shida zao, wewe unasubiri nini? Rudini CCM, na nawapongeza wote mliojiunga na CCM, viongozi pamoja na wanachama. Karibuni sana tufanye kazi ya kujenga taifa pamoja.”
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages