Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Tanzania inapeleka mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro ili kuitangazia dunia kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni imara na pia itaendelea kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, Waziri Ridhiwani Kikwete amesema kuwa kwa mwaka huu 2024, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamru mwenge wa uhuru upelekwe juu ya mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio zake kwa siku 195.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo Oktoba 15, 2024 katika hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wakati wa hafla ya kupokea kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambacho kimepewa jukumu la kupeleka Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania kilele cha mlima Kilimanjaro.
Vile vile, Waziri Ridhiwani Kikwete amehamasisha vijana kuendelea kuenzi falsafa za mwenge wa uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961.
Awali akizungumza, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kupandishwa mwenge wa uhuru mlima Kilimanjaro mwaka huu 2024 kunaleta hamasa ya uzalendo kwa wananchi hususan wakati huu ambao Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya uhuru na mafanikio ya Taifa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia mwenge wa uhuru kupandishwa kwa mara nyingine katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Kiongozi wa hicho Maalum, Luteni Kanali Khalid Khamis Khalid amemhakikishia Mhe. Waziri Ridhiwani Kikwete kuwa kikosi hicho kitaulinda, kuutunza na kuufikisha Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa la Tanzania katika kilele cha mlima huo wa Kilimanjaro.