Breaking

Monday, 21 October 2024

MHE. PINDA AFUNGA MAFUNZO MAALUM KWA WAANGALIZI WA UCHAGUZI WA SADC

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (𝗦𝗔𝗗𝗖- SEOM) Mhe. Mizengo Pinda amefunga mafunzo maalum yaliyoendeshwa na Secretariet ya SADC kwa waangalizi wa misheni hiyo wanaotoka katika nchi wanachama wa SADC.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mhe. Pinda amewasihi waangalizi hao kuhakikisha wanazingatia misingi na miongozo yote waliyopatiwa wakati wa mafunzo na hivyo kutekeleza jukumu la uangalizi kwa mafanikio.

“Mmekuwa hapa kwa muda wa siku nne, ni matumaini yangu kuwa mmeelewa na mtazingatia mafunzo mliopewa, niwasihi muhakikishe mnafuata na kuzingatia misingi na miongozo mliyopewa na waendesha mafunzo, mjue kuwa sasa kazi imeanza na kilichobaki ni kutekeleza jukumu la uangalizi ambalo lipo mbele yetu,” alisema Mhe. Pinda.

SADC iliendesha mafunzo ya siku nne kwa waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya hiyo katika uchaguzi Mkuu wa Botswana unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024. Mafunzo hayo maalum kwa Misheni ya SEOM yalifanyika jijini Gaborone, Botswana kuanzia tarehe 17 hadi 20 Oktoba 2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uangalizi wa Uchaguzi huo Mkuu.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Sekretarieti ya SADC na Taasisi ya Uchaguzi kwa Demokrasia Endelevu Afrika (EISA), yaliangazia masuala mbalimbali ya kisera na kisheria ya Botswana, kikanda na kimataifa ambayo hutumika kusimamia uchaguzi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia na utawala bora katika ukanda wa SADC.

Mafunzo hayo yamewapatia waangalizi maarifa na kuwawezesha kufahamu viwango na kanuni za uchaguzi za kidemokrasia; Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia iliyorekebishwa; uangalizi wa uchaguzi katika hali za dharura za afya ya umma (mfano janga la COVID-19); kukuza uelewa kuhusu mzunguko wa uchaguzi; tathmini ya hatua za mzunguko wa uchaguzi; mifumo ya uchaguzi katika kanda ya SADC; ujuzi wa ukusanyaji taarifa; na matumizi ya vishikwambi, pamoja na ukusanyaji na utumaji wa taarifa (data).

Katika Uchaguzi mkuu huo wananchi wa Botswana watachagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambapo viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa. SEOM inatarajiwa kupeleka waangalizi wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages