Breaking

Tuesday, 29 October 2024

MAELEKEZO YA WAZIRI BASHUNGWA YATEKELEZWA, MV. KILINDONI YAANZA KUTOA HUDUMA

“Msitoke Mafia mpaka Kivuko kianze kutoa huduma kwa Wananchi,”

Hiyo ni kauli ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa aliyoitoa siku ya Tarehe 26 Oktoba, 2024 alipokuwa Wilayani Mafia Mkoani Pwani katika ziara ya kikazi ambapo alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi. Aisha Amour kumuagiza aambatane na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala wakapige kambi katika Kisiwa cha Mafia kusimamia matengenezo ya Kivuko MV. KILINDONI na kuhakikisha hawatoki mpaka huduma ya usafiri wa kivuko kati ya Nyamisati na Mafia inarejea kwa wananchi.

Maelekezo hayo yametekelezwa kwa usahihi, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Charles Msonde alifika eneo hilo kutekeleza maelekezo ya Waziri Bashungwa akiambatana na Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro Kilahala na kushuhudia mafundi wa Wakala huo wakipambana kuhakikisha kivuko hicho kinarejea haraka kutoa huduma.

Kivuko hicho kilifanikiwa kutengemaa na hatimaye kimeanza kutoa huduma siku ya Jumapili baada ya kufanyiwa majaribio ya takribani masaa manne na kuonekana kiko tayari ambapo kilifanikiwa kurejea kutoa huduma kwa kusafiri kutoka Nyamisati kuelekea Mafia siku hiyo hiyo majira ya saa mbili za usiku kikiwa na abiria pamoja na mizigo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Mafia wametoa shukran zao za dhati kwa Waziri wa Ujenzi kwa kuwahakikishia kivuko kinarejea kuwapatia huduma kwani kivuko hicho ndio usafiri pekee wanaoutegemea kusafirisha bidhaa zao.

Mussa Seif mkazi wa Kisiwa cha Mafia amesema anaishukuru Serikali kwa juhudi ilizofanya kuhakikisha kivuko hicho kinarejea kutoa huduma.

Naye Mohamed Mswala ambaye pia ni mkazi wa visiwani humo amesema anashukuru kwa juhudi kubwa za Serikali ambazo zimezaa matunda na kurejesha huduma hiyo kwa wananchi wa Mafia, ‘’alikuja Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye anahusika na kivuko hiki akaweka timu maalumu ikimhusisha Katibu Mkuu wa Wizara kuhakikisha kivuko kinarudi katika hali yake, ndani ya siku mbili hizi, ilikuwa Tarehe 26, leo tunashukuru Mungu zile ahadi alizozungumza na wakazi wa Mafia zimekwenda vizuri na wameitekeleza kwa wakati,’’

Amesema mkazi huyo huku akiendelea kutoa shukran kwa juhudi kubwa zilizofanyika kurejesha huduma hiyo ya kivuko ambazo zimeonyesha namna Serikali inavyowajali wananchi wake.

Hassan Yusuph ambaye anafanya kazi ya kubeba mizigo katika kivuko hicho pia, ametoa shukrani za dhati kwa Rais Samia kwa jitihada zake ambazo zimewafikisha hatua hiyo ikiwemo kuwapelekea kivuko hicho na pia kuanza ujenzi wa kivuko kipya ambacho kitaenda kuongeza nguvu ya utoaji huduma eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Abdulrahman Ameir amesema kivuko hicho kinatarajiwa kusafiri tena usiku wa Tarehe 29 Oktoba saa saba za usiku kurejea Nyamisati kikiwa na abiria pamoja na mizigo yao, Mhandisi Ameir amewaomba radhi wakazi wa maeneo hayo kwa kipindi chote ambacho kivuko hicho hakikuweza kutoa huduma.

Kivuko MV. KILINDONI kilipata hitilafu tangia siku ya Tarehe 10 Oktoba, 2024 na kupelekea Wananchi wa kisiwa hicho kukosa huduma ya vivuko hali iliyowapelekea kutumia vyombo vya usafiri visivyo salama na vya uhakika.

Serikali katika kutatua kero za namna hiyo, tayari imeanza ujenzi wa kivuko kipya kikubwa zaidi ambacho mpaka sasa ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 35, kivuko hicho kinagharimu Shilingi Bilioni 9 na kitakapokamilika kitafanya idadi ya vivuko katika eneo hilo kuwa vitatu.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages