Breaking

Saturday, 12 October 2024

DKT. SHEKALAGHE AHIMIZA SHIUMA KUWA KITU KIMOJA KWA MAENDELEO YA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO

Na WMJJWM, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe amewataka viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) ngazi ya Taifa na mikoa kuwa kitu kimoja na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zinazosimamiwa na Serikali kwa maendelea ya wafanyabiashara ndogondogo nchini.

Hayo ameyasema Oktoba 11, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu miongozo ya uratibu wa utoaji mikopo kwa viongozi wa SHIUMA, ili waweze kushirikiana na Serikali katika kutoa hamasa na elimu kwa ŵafanyabiashara ndogondogo kuendelea kujitokeza kujisajili kwenye Mfumo wa Kidigitali wa Kusajili Wafanyabiashara Ndogondogo (WFB).

"Baada ya mafunzo haya, ni matarajio yangu kuwa, juhudi zenu za kutoa hamasa kwa wafanyabiashara ndogondogo litazaa matunda tunapoelekea kwenye uzinduzi wa Vitambulisho na Mikopo yenye mashart nafuu itakayoanza kutolewa na Serikali kupitia Benki ya NMB na kitambulisho cha kidigitali kitakuwa moja ya dhamana yako", amesema Dkt. Shekalaghe.

Ameongeza kuwa, Wafanyabiashara ndogondogo wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, akisisitiza kwamba, Dhamira ya Serikali ya kutoa vitambulisho hivyo imeambatana na faida nyingi zikiwemo kutambulika na taasisi mbalimbali, kuunganishwa na mifumo ya NIDA, NAPA na Huduma nyingine za kijamii.

Aidha, Dkt. Shekilaghe amewaasa viongozi wa SHIUMA kuendelea kuwa wazalendo na kuwa mfano mzuri na watakaporejea watoe mrejesho kwa wafanyabiashara ndogondogo, pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwa upande wa mwenyekiti wa SHIUMA mkoa wa Pwani Filemon Maliga , amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuwatambuwa, kuboresha mazingira ya wao kufanya kazi kwa umoja pamoja na kuwapambania kuwaunganisha na taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Uzinduzi wa utambuzi na usajili wa vitambulisho vya kidijitali unatarajiwa kufanyika Otoba 17, 2024 jijini Arusha.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages