Breaking

Saturday, 5 October 2024

DAUDI ATOA RAI KWA TAASISI ZA UMMA KUTUMIA MFUMO WA e-MREJESHO KUPOKEA KERO ZA WANANCHI

 

Na Mwandishi Wetu

Oktoba 4, 2024

Taasisi za Umma zimetakiwa kutumia mfumo wa e-Mrejesho na kuhakikisha kero zote zinazowasilishwa katika mfumo huo zinafanyiwa kazi na wahusika wanapewa majibu  kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi wakati akifunga kikao kazi cha kukusanya maoni ya maboresho ya mfumo wa e-Mrejesho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam.

"Nitumie fursa hii kutoa rai kwa Maafisa Masuuli wote wa Taasisi za Umma ambao taasisi zao hazijaanza kutumia mfumo wa e-Mrejesho, kuhakikisha wanajiunga katika mfumo huo kabla ya kumalizika kwa mwezi huu wa Oktoba, 2024" alisisitiza Daudi.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma  na Utawala Bora Idara ya Usimamizi wa Maadili kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao, imetengeneza mfumo wa e-Mrejesho kwa lengo la kuwasaidia wananchi kuwasilisha maoni, maulizo, hoja, malalamiko na pongezi kwa Serikali kwa urahisi, haraka na gharama nafuu. Hivyo, kushindwa kujiunga na mfumo huo ni kuwanyima kwa makusudi wananchi haki ya kusikilizwa na kutatuliwa kero.

Aidha, Bw. Daudi amewataka viongozi wa taasisi zote za Umma kuhakikisha wanazingatia maekelezo hayo na wanaimarisha dawati la mrejesho kwa kuweka watumishi wenye weledi na wanaoweza kutunza siri wanaposhughulikia maoni, hoja na malalamiko ya wananchi.

Vilevile, amewataka viongozi wa Taasisi za Umma kuhakikisha maofisa mrejesho wote wanapatiwa mafunzo mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali zinazowasilishwa kwenye dawati hilo la mrejesho.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Leila Mavika, amesema Idara imejipanga kutoa mafunzo kwa watumishi wote wanaosimamia mfumo, ingawa kwa awamu hii ya kwanza jumla ya Maafisa TEHAMA na maafisa mrejesho wapatao 105 ambao taasisi zao zinafanya vizuri katika kutumia mfumo wa e-Mrejesho wamepitishwa katika mfumo na kutoa maoni ya maboresho. 

Aidha, Bi. Mavika amesema kuwa mfumo wa e-Mrejesho unafanya kazi kwa ufanisi na unapatikana wakati wote kupitia simu za mkononi *152*00#, apilikesheni ya emrejesho au tovuti www.emrejesho.gov.go.tz.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Udhibuti na Usalama wa Mifumo ya TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bw. Sylvan Shayo amesema e-GA ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora kuhakikisha maoni na maboresho yote yaliyotolewa  na wadau yanafanyiwa kazi.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages