Na Mwandishi Wetu, Kigoma
WANANCHI wameshauriwa kabla ya kununua bidhaa wahakikishe wanasoma kwa umakini taarifa zilizopo kwenye vifungashio ili kujiridhisha kama bidhaa hizo zimethibitishwa ubora na kama hazijaisha muda wake wa matumizi pamoja na taarifa zingine za msingi kwa lengo la kulinda afya zao.
Ushauri huo ulitolewa na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwenye mwendelezo wa kampeni ya elimu kwa umma illiyotolewa mkoani Kigoma katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya za Buhigwe, Uvinza na Kasulu kuanzia tarehe 09 Septemba HADI 20 Septemba 2024.
Miongoni mwa waliofikiwa na elimu hiyo ni wananchi wapatao 2,730 wakiwemo wajasiriamali 110.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hao jana, Afisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Deborah Haule, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora, jinsi ya kutoa taarifa za bidhaa hafifu pamoja na zile ambazo hazijaisha muda wake wa matumizi.
Kwa upande wa wajasiriamali, Haule alisema kupitia kampeni hiyo Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na uchumi wao binafsi inathibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha bure, hivyo wanatoa elimu kwao ili wachangamkie fursa hiyo.
Haule alisema mashirika ya viwango ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yameingia makubaliano ambapo bidhaa ikishapimwa na kuthibitishwa na shirika la viwango la nchi husika ikivuka mipaka na kwenda nchi nyingine, haitakiwi kupimwa tena.
"Kwa hiyo hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wanaothibitisha bidhaa zao wanaotakiwa ni kuja na barua ya utambulisho kutoka SIDO hatutaki kumuacha nyuma mjasiriamali yeyote, kwa kufanya hivyo tutainua uchumi wao na wa nchi kwa ujumla," alisisitiza
Aisema TBS inatoa elimu hiyo kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa viwango ili kulinda afya za walaji na kuwawezesha wazalishaji wa bidhaa kiuhimili soko la ndani na nje ya nchi.
'Tunataka wananchi waache kununua bidhaa kwa mazoea na badala yake waangalie muda wake wa mwisho wa matumizi na pindi wakikutana na bidhaa ambazo hazina ubora, au zimeisha muda wake wa matumizi au kutilia mashaka bidhaa yoyote wasisite kuwasiliana na TBS kupitia namba ya bure ya Kituo cha Huduma kwa Hateja," alisema.
Alisema matakwa ya ubora ni pamoja na bidhaa kuwa na tarehe ya mwisho wa matumizi, hivyo kupitia kampeni hiyo wanaelimisha jamii na wadau kwa ujumla taarifa za kuzingatia kwenye vifungashio kabla ya kununua bidhaa.
"Kupitia kampeni hii wataalam wa TBS walipita katika maeneo ya mikusanyiko, maduka, kwenye vikundi vya wajasiriamali na kutoa elimu za kuhifadhi bidhaa na namna ya kutumia alama za viwango vya TBS ili kutambua ubora wa bidhaa hizo," alisisitiza
Alisema elimu hiyo inatolewa kwa wananchi kupitia maeneo ya wazi, ikiwemo minadani , stendi, masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya atu wengi.
Aliendelea kusema kwamba TBS inatambua mchango wa jamii katika kupigana vita dhidi ya bidhaa hafifu na ndio maana inafanya kampeni hii ili kuunganisha nguvu za pamoja ili kuwa na Tanzania isiyokuwa na bidhaa hafifu kwenye sokoni.
Naye Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TBS, Peter Musiba, aliwataka wafanyabiashara kujitokeza kusajili majengo ya vyakula na vipodozi ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji.
“Tunatoa wito kwa wafanyabiashara kusajili majengo ya vyakula na vipodozi, kwani ni takwa la kisheria," alisema Musiba.
Kwa upande wa usajili wa bidhaa , Musiba alisema eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi.