Breaking

Tuesday, 17 September 2024

WANANCHI WAHAMASISHWA KUJITOKEZA SEPT.23 KILELE CHA TAMASHA LA UTAMADUNI



Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro,akizungumza kuhusu Tamasha la tatu la utamaduni kitaifa litakaloanza Septemba 20-23, mwaka huu na siku ya kilele kitafanyika uwanja wa majimaji na Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Wananchi wakiwa kwenye kaburi la Chifu wa Wangoni Nkusi Mharule Bin Zulu Gama wakihiji kama sehemu ya kuendeleza mila na desturi za kingoni.

Wananchi wakicheza ngoma ya Lizombe ambayo ni moja ya ngoma za utamaduni wa wangoni.


Na Mwandishi Wetu, DOODMA


WAGENI zaidi ya 5,000 wanatarajiwa kushiriki katika Tamasha la tatu la utamaduni kitaifa litakalofanyika Septemba 20-23, mwaka huu mkoani Ruvuma huku wananchi wakitakiwa kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Songea, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro alisema tamasha hilo litaanza Septemba 20-23, mwaka huu na siku ya kilele kitafanyika uwanja wa majimaji na Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Alisema tamasha hilo litajumuisha maonesho ya mavazi ya asili ikiwamo kanga, vyakula, ngoma kama vile Mganda na Lizombe.

Alibainisha kuwa Rais atakutana na wazee wa kimila na kuzungumza nao kwa kuwa mkoa huo unahistoria mbalimbali kama vile vita ya majimaji kwa kutembelea kaburi la halaiki la mashujaa wa majimaji.

“Wanasongea na wanaruvuma tumepewa fursa hii tukifanikisha ndio fursa nyingine tena kwetu, na baada ya hapo Rais ataendelea na ziara mkoa mzima kwenye wilaya zote sita,”alisema.

Alisema Rais Samia atahitimisha ziara yake Septemba 28, mwaka huu kwa kufanya mkutano wa ndani wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na mkutano wa hadhara kwa wananchi kwenye uwanja wa majimaji.

Naye, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, Meliud Mwampembe, alisema shule hiyo imetoa kipaumbele kwa masuala ya michezo na utamaduni kwa wanafunzi.

“Hili jambo la utamaduni na michezo ni la msingi kwasababu linatunza asili yetu sisi kama watanzania, ninahamasisha sana wananchi kushiriki katika tamasha hili linaloonesha tamaduni zetu lakini na fursa mbalimbali zilizopo Ruvuma,”alisema.

WAWEKEZAJI WAITWA

Katika hatua nyingine, wawekezaji nchini wameombwa kuchangamkia fursa ya kuwekeza mkoani Ruvuma kutokana na kuwapo na vivutio mbalimbali ikiwamo kaburi la Chifu wa Wangoni aliyezikwa na wasaidizi wake wawili wakiwa hai.

Akizungumza jana mkoani humo katika kuelekea Tamasha hilo, Msimamizi wa eneo hilo kaburi la Chifu huyo aliyefahamika kwa jina la Nkusi Mharule bin Zulu Gama alitawala wagoni mwaka 1874-1889, Agnes Ngonyani alisema katika kaburi hilo amekuwa akipokea wageni kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kuzulu.

“Katika eneo hili zimetengwa heka nane tunawakaribisha wawekezaji kupitia Rais wetu Samia Suluhu Hassan waje kuwekeza eneo hili kwa kufanya mambo mbalimbali ya kuinua mil ana desturi zetu zilizoachwa na mababu zetu,”alisema.

Alisema kwa tamaduni zao kila mwaka wangoni wamekuwa wakihiji kwenye kaburi hilo kuomba baraka kwa kiongozi wao.

“Katika kaburi hili huyu chifu alizikwa na watu wawili wakiwa wazima na hao watu walikuwa wasaidizi wake na wala hawakukamatwa kwa ubabe waliambiwa wewe na wewe tunakwenda kuwazika pamoja na chifu na walipopokea ujumbe huo walifurahia ni jambo jema kuzikwa na chifu.”

“Umaarufu wa kaburi hili pia kuna nyoka mkubwa haonekani mara kwa mara, baada ya miaka mitano au 10 huenda huko bondeni kunywa maji mimi hadi umri huu sijawahi kumuona ila kuna watu wameshawahi kubahatika kumuona,”alisema.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages