Breaking

Tuesday, 17 September 2024

WAKILI KULAYA: KUNA FAIDA KUBWA SANA WANAWAKE KUWA VIONGOZI


Ili nchi iweze kuendelea ni lazima vijana na wanawake ambao ndio kundi kubwa la watu hapa nchini wawe viongozi na kwamba kukosekana kwa viongozi katoka kwenye kundi hilo ambalo idadi yake ni kubwa kwa mujibu wa ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 kutafanya kuendelea kubaki ilipo bila kupiga hatua na hatimaye kuifanya nchi ya Tanzania kuwa Taifa masikini.

Miongoni mwa faida kubwa sana kwa jamii na taifa pindi wanawake wanapokuwa viongozi ni pamoja na kusaidia kuongeza nguvu na maarifa ya kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia, ubaguzi na kuinufaisha jamii kwa ujumla wake.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo Septemba 17, 2024 na Mratibu wa Taifa wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) Wakili Anna Kulaya akifungua mafunzo ya wanawake watia nia.

Wakili Kulaya ameongeza kwa kusema kuwa, jamii kwa ujumla hususani wanaume wanapaswa kueleza umma kuwa, wanawake wana haki sawa ya kuwa viongozi sawa sawa na ilivyo kwa wanaume.

Ameendelea kwa kusema kuwa, kuna fikra mbaya na hasi kwa jamii ya kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi na kutaka jamii kuondokana na fikra hizo potofu.

Akiongelea kuhusu suala la kufanikwa katika uongozi misingi ambayo mwanamke anapaswa kuifuata ili kufanikiwa, Wakili Kulaya amesema "Ili kuwa kiongozi inakupasa kwanza kuwa na dhamira ya dhati kutoka moyoni mwako ukiamini kabisa kuwa mimi nataka kuongoza, na ujue ni kwa nini unataka kuongoza" alisema na kuongeza

"Naomba wanaume muwasapoti wanawake pale wanaposhiriki kwenye michakato ya uchaguzi kwa namna moja au nyingine ikiwemo kuchukua fomu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi."

Katika hatua nyingine amewasihi wananchi kushiriki katika zoezi la kujiandikisha pamoja na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwani kupitia hilo ndipo haki ya kuchagua na kuchaguliwa inapatikana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye ni mwezeshaji katika mafunzo hayo amesema, mafunzo hayo yatawanufaisha washiriki na kuwabadilisha kifkra na kimtazamo na kuwafanya washiriki kubaini changamoto zilizowakuta watia nia katika chaguzi zilizopita na kuzitafutia ufumbuzi ikiwa na kupaza sauti ili changamoto hizo zisitokee tena katika chaguzi zijazo na kwa yale mambo mazuri basi uzoefu huo ushirikishwe kwa wanawake watia wapya.

Mafunzo hayo ya siku 4 yanafanyika chini ya Mradi wa WILDAF ujulikanao kama Wanawake Sasa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland na yanalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) limekuwa likitumia sheria kama nyenzo muhimu ya kumkomboa mwanamke katika nyanja mbalimbali ikiwemo kisasa, kiuchumi, kiutamaduni, kiteknolojia.

WiLDAF imekuwa ikifanya hivyo kwa kuamini kwamba kukiwa na sheria nzuri na wezeshi kutawafanya wanawake waweze kumiliki au kunufaika na fursa zinazotokana na rasilimali mbalimbali huku shabaha kubwa ikiwa ni kuhakikisha wanawake wanashiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages