Breaking

Thursday, 19 September 2024

UJENZI WA BANDARI YA MBAMBABAY KUIFUNGUA RUVUMA KIUCHUMI



Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mbambabay utakaogharimu Sh.Bilioni 81, utaufungua Mkoa kiuchumi kwa kuuza bidhaa mbalimbali nchi za Malawi na Msumbiji.

Kanali Ahmed aliyasema hayo jana alipokuwa akikagua utayari wa Wilaya za Mkoa huo kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan na kilele cha Tamasha la Kitaifa la tatu la Utamaduni litakalofanyika uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea.

Alisema serikali imeelekeza fedha hizo zitekeleze mradi huo ikiwa ni miongoni mwa miradi mikubwa itakayoipaisha Ruvuma kiuchumi.

Alisema ujenzi wa bandari hiyo ukikamilika utasaidia kutoa ajira, kuinua uchumi, kupeleka na kupokea bidhaa mbalimbali ikiwamo mazao, samaki na bidhaa za viwandani katika nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

“Tunamshukuru Rais kwa kuleta fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa wananchi wetu kwenye sekta ya afya, elimu, miundombinu kama unavyoona hapa kutajengwa bandari hii ambayo Sh.Bilioni 81 zimetolewa kutekeleza mradi huu,”alisema.

Aidha, Mkuu huyo alikagua barabara ya Mbinga hadi Mbambay ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami na kwamba barabara hiyo itafungua uchumi wa mkoa huo kwa kuwa ni kiunganishi kati ya Tanzania, Malawi na Msumbiji.

Alisema mkoa huo umejiandaa kumpokea Rais Samia katika ziara yake itakayoambatana na matukio mbalimbali ikiwamo Tamasha hilo.

“Rais anakuja kwa mara ya kwanza tangu awe Rais wa Tanzania, pia anakuja kwenye tamasha la kitaifa ambalo sisi Ruvuma tumechaguliwa tuwe wenyeji wa hili na kama unavyofahamu ni Mkoa umesheheni tamaduni nyingi,”alisema.

Alibainisha kuwa ziara hiyo ya Rais inalenga kukagua miradi ambayo mkoa huo umepokea fedha nyingi kuitekeleza katika sekta mbalimbali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages