Breaking

Thursday 19 September 2024

NG'UMBI AWATAKA WADAU KUONGEZA USHIRIKIANO KATIKA ELIMU


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi akifafanua jambo wakati wa mahojiano maalum kuhusu hali ya elimu nchini kupitia kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kilichorushwa na Radio One leo Septemba 19, 2024.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi akiandika maswali ya wananchi wakati wa kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kilichorushwa na Radio One leo Septemba 19, 2024.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi akiongea wakati wa mahojiano maalum kuhusu hali ya elimu nchini kupitia kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kilichorushwa na Radio One Stereo leo Septemba 19, 2024.


Na Mwandishi Wetu


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi ametoa wito kwa wadau wa elimu kutoka sekta binafsi, washirika wa maendeleo na jamii kuongeza ushirikiano wao kwa Serikali ya Awamu ya Sita ili kuboresha na kupanua zaidi fursa za elimu nchini.

Pia, amewahimiza watanzania kutumia fursa kubwa ya kupata elimu kwa njia mbadala kupitia TEWW, ambapo huduma zake zinapatikana kote nchini.

Kiongozi huyo ameyasema hayo leo Septemba 19, 2024 katika mahojiano maalum kuhusu hali ya elimu nchini kupitia kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kinachorushwa mbashara na Radio One Stereo.

Katika mahojiano hayo, Profesa Ng’umbi amebainisha kuwa Tanzania inaweza kufikia kiwango cha kimataifa cha idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika cha asilimia 87 kutoka ilipo hivi sasa (asilimia 83) iwapo wadau wote wa elimu wataongeza ushirikiano.

“Ushirikiano ni muhimu sana, wazazi wahakikishe watoto wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na wanabaki shuleni hadi wamalize masomo...wadau binafsi na wadau wa maendeleo wana nafasi kubwa ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma ya elimu inawafikia watu wote bila ya kumwacha mtu yeyote,” amesema.

Kulingana na taarifa ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) asilimia 17 ya watanzania hawajui kusoma na kuandika, na Mikoa ya Tabora, Rukwa, Simiyu, Dodoma na Katavi ndiyo yenye idadi kubwa ya watu hao.

Kwa mujibu wa Profesa Ng’umbi pamoja na mambo mengine, hali hiyo imechangiwa kwa kiwango kikubwa na watoto wenye umri wa kwenda shule kutoandikishwa kwa asilimia 100, na kuacha masomo kwa sababu mbalimbali; ikiwemo utoro, mimba za utoto na nyinginezo.

Wakati huo huo, Mkuu huyo wa TEWW amewataka watanzania wenye sifa za kujiunga na mafunzo yanayotolewa na taasisi yake ya ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada kuchangamkia fursa kabla dirisha halijafugwa.

Kwa taarifa zaidi amewataka watembelee tovuti ya taasisi (www.iae.ac.tz) au wapige simu zifuatazo: Dar es Salaam Main Campus (0754 606 455/0713 238 806); Mwanza Campus (0717 110 180/0744 336 697); Morogoro Campus (0784 239 999/0683 076 665); na Ruvuma Campus (0654 832 026/0784 591 344).
TEWW ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 12 ya mwaka 1975, yenye jukumu mahususi la kutoa elimu ya kujiendeleza na mafunzo ya elimu ya watu wazima kupitia mfumo usio rasmi, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu, wawezeshaji, na wasimamizi wa elimu ya watu wazima nchini.

Taasisi hii ilisajiliwa rasmi na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (National Council for Technical Education – TACTE) mwaka 2005 na kupata ithibati kamili mwaka 2009 ya kutoa mafunzo kwa walimu na waendeshaji wa elimu ya watu wazima katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada.

TEWW inatoa pia elimu ya sekondari kwa vijana nje ya shule, wafanyakazi na watu wazima ambao wanajiendeleza kupitia mfumo wa elimu kwa njia mbadala kwa kutumia njia ya elimu masafa (distance learning) na ana kwa ana.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages