Breaking

Wednesday, 18 September 2024

DKT. KIRUSWA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI, ATATUA MGOGORO



Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameshuhudia Utiaji Saini wa Mikataba ya usambazaji na utoaji wa huduma mgodini katika mgodi wa uchimbaji Madini ya Urani uliopo katika Kijiji cha Likuyu kilichopo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.

Mikataba hiyo imesainiwa Septemba 18, 2024 ambayo imehusisha Kampuni ya Ako Group Tanzania Limited ambayo ni mzabuni wa Kampuni ya Mantra na vikundi vilivyoundwa na wazawa vitakavyo toa mahitaji mbalimbali kwa mzabuni huyo. Ako Group wanatoa huduma ya chakula na usafi katika mradi huo, hivyo mikataba hiyo itasaidia ununuzi wa mahitaji muhimu ya chakula na usafi kufanyika ndani ya Wilaya ya Namtumbo na kukuza uchumi wa jamii hiyo.

Aidha, Dkt. Kiruswa amekagua maendeleo ya mradi wa uchimbaji Madini ya Urani katika mgodi wa Mantra ambapo ameridhishwa na maendeleo ya mradi na kuahidi kushughulikia mikwamo iliyopo kwa haraka ili uzalishaji wa madini hayo uanze kama inavyo tarajiwa.

Naye, Meneja wa Uendelevu Mradi wa Mantra, Majani Wambura amesema mpaka sasa mradi huo umetumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 240 katika ujenzi wa mradi na inategemewa mpaka kukamilika kwake dola za Kimarekani zaidi ya bilioni moja zitatumika na ajira zaidi ya 700 zitatengenezwa kwa jamii.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa ametatua na kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya Kampuni ya Mantra na Kikundi cha Kuza Uchumi wa Namtumbo (KUNA) ambacho kinadai fidia ya eneo ulipo mradi kwasasa, wakidai kuwa eneo hilo lilikiwa linamilikiwa na babu zao ambao waliondolewa kwa nguvu na Wakoloni kati ya mwaka 1940 - 1945 na baadae eneo kutwaliwa na Serikali na kulifanya kuwa hifadhi ya Taifa.

Dkt. Kiruswa amesema fidia ni haki ya Kisheria kwa mtu atakaye hamishwa katika eneo lake kupisha mradi, hata hivyo, madai ya fidia ya Kikundi hiki hayana msingi thabiti wa Kisheria kama ulivyo wasilishwa, hivyo amewashauri wanakikundi hao kuangalia kwa upana faida watakazo nufaika nazo kwa uwepo wa mradi huu ikiwa ni pamoja na fursa ya Kisheria ya wajibu wa Mmiliki wa Leseni kwa Jamii (CSR) pamoja na Ushiriki wa Watanzania kwenye Uchumi wa Madini (Local Content).

Aidha, Dkt. Kiruswa amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za madini Mkoani humo ambapo ameupongeza Mkoa huo kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa asilimia 119 katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2024/25.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Abbas amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kufanya ziara Mkoani humo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.

Awali, Dkt. Kiruswa aliungana na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa kukagua ujenzi wa miundombinu ya Uwanja wa Ndege inayoendelea Mkoani humo iliyoghalimu kiasi cha shilingi bilioni 37 ambapo maboresho yaliyofanyika ni pamoja na jengo la kuongoza ndege, uzio wa uwanja, taa za kuongoza ndege, eneo la urukaji wa ndege na lami katika barabara za uwanja wa ndege.







Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages