Breaking

Friday, 20 September 2024

CCM YASISITIZA UHUSIANO WA KIMATAIFA KUIMARISHA UCHUMI NA MAENDELEO YA WATU


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa Serikali na Nchi ya Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa wenye manufaa ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Balozi Nchimbi amesema kuwa urafiki na uhusiano wa kidiplomasia unapaswa kuendelea kuwa mojawapo ya njia sahihi katika kuboresha ushirikiano wa pande mbili kimataifa, kati ya nchi na nchi, au nchi na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema hayo alipokutana na mabalozi wanaowakilishi nchi zao hapa nchini, kutoka nchi za Brazil na India, pamoja na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje ya Chama Tawala cha Msumbiji (FRELIMO) na Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Friedrich Ebert Stiftung (FES), nchini Tanzania.

Katika mazungumzo na viongozi hao, yaliyofanyika kwa nyakati tofauti tofauti, leo 19 Septemba 2024, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, Balozi Nchimbi amesema mojawapo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM unaofanywa na Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kuendelea kuboresha uhusiano wa kimataifa, hasa kupitia diplomasia ya uchumi, kwa ajili ya kuimarisha uchumi, maendeleo ya watu na kubadilishana uzoefu kwenye uongozi na demokrasia.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Mhe. Gustavo Martins Nogueira na Balozi Nchimbi, viongozi wote wawili walionesha msisitizo na utayari wa kuendelea kuboresha uhusiano kati ya Tanzania na Brazil kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili, hasa katika nyanja za afya, kilimo na michezo.

Kwenye mazungumzo ya Balozi Nchimbi na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey, viongozi hao wamezungumzia umuhimu wa kuendelea kuenzi ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali, zikiwemo teknolojia, biashara na elimu, ikizingatiwa India ni mojawapo ya nchi zilizopiga hatua kubwa za kimaendeleo katika maeneo hayo.

Katika mazungumzo ya Balozi Nchimbi na Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa wa FRELIMO, Komredi Alcinda Antonio de Abreu, pande zote mbili zimesema urafiki na udugu wa damu uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji utaendelea kuenziwa kwa kushirikiana kadri inavyohitajika, kama ilivyo ada tangu wakati wa kupigania ukombozi wa kisiasa wa Nchi za Kusini mwa Afrika, na sasa mkazo umeelekezwa kwenye ukombozi wa kiuchumi na kuendelea kuboresha hali za maisha ya watu.

Aidha, katika mkutano wa Balozi Nchimbi na Mkurugenzi Mkaazi wa FES nchini Tanzania, Bwana Christian Denzin, ambaye alimtembelea Katibu Mkuu wa CCM kwa ajili ya kujitambulisha, pande zote mbili zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya CCM na shirika hilo la nchini Ujerumani, hasa katika kuimarisha uwezo na uzoefu katika nyanja za uongozi na demokrasi, kupitia miradi mbalimbali ya mafunzo ya viongozi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages