Breaking

Wednesday, 28 August 2024

WILDAF YAJIPANGA KUWAPIGA MSASA WATIA NIA WANAWAKE

  

Na Rose Ngunangwa - Dar es salaam

Jamii imeaswa kuhakikisha kwamba wanaume na wanawake wanashirikiana ili taifa lisonge mbele kimaendeleo.

Wito huo umetolewa  na Mratibu wa Taifa wa WILDAF Wakili Anna Kulaya wakati akifungua mafunzo katika warsha ya kuwajengea uwezo waraghabishi ambao watakwenda kufanya mafunzo kwa wanawake watia nia yaliyoanza leo jijini Dar es Salaam.

Katika kazi zetu tuligundua kwamba jamii haina shida ya kuwapigia kura viongozi wanawake lakini changamoto kubwa ilikuwepo kwenye michakato ya vyama ambako majina ya wanawake watia nia yalikuwa yakikatwa.

Wakili Kulaya alishukuru uwepo wa mabadiliko kwenye sheria za uchaguzi ambayo yanasisitiza masuala ya jinsia katika ngazi zote za vyama vya siasa na kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchaguzi na ngazi za maamuzi.

Kwa upande wake, Dkt. Helen Kijo Bissimba ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha wanawake watia nia umuhimu wa kuleta mabadiliko katika jamii yao pamoja na kutumia medani za uwezeshaji wa namna ya kuongea na hadhira.

“Ukatili wa kijinsia hushamiri sana wakati wa uchaguzi ikiwemo rushwa ya ngono. Upo umuhimu wa kuwajengea uwezo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kukabiliana na ukatili na kuongeza ushiriki wao katika chaguzi,” alisema.

Mafunzo haya yanafanyika chini ya Mradi wa WILDAF ujulikanao kama Wanawake Sasa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland na yanalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi katika ngazi za maamuzi.

Watanzania wanatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba mwaka 2024.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages