Breaking

Tuesday 27 August 2024

WAZIRI AWESO ATIKISA MTAA KWA MTAA DAR




Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezindua rasmi kampeni ya Mtaa kwa Mtaa katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA na kuiagiza Mamlaka zote za Maji Nchini kutekeleza kampeni kikamilifu kwa kuwashirikisha wananchi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wateja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Kata ya Kunduchi katika mtaa wa Tegeta, jijini Dar es Salaam Mhe. Aweso amesema lengo la kampeni hii ni kuhakikisha wananchi wanasikilizwa changamoto walizonazo za upatikanaji wa huduma ya majisafi na kutatuliwa kikamilifu.

Ameiagiza DAWASA kutekeleza zoezi hili kwa ufanisi na kuelekeza nguvu kwenye maeneo ya wateja ambayo hayana huduma ya maji na sio tu kwa wateja wenye maji.

Mhe. Aweso ameongeza kuwa katika kampeni hiyo Mamlaka za Maji zihakikishe wateja wote waliokamilisha malipo ya kupata maunganisho mapya ya maji wapewe kipaumbele na waweze kuunganishwa na huduma ya majisafi.

"Watu wasiteseke kupata huduma ya maji na pale panapokuwa na ulazima wa kusitisha huduma kwa muda, wateja wapewe taarifa mapema ili waweke akiba ya maji mapema," ameeleza Mhe Aweso.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa Mamlaka imepokea maelekezo ya Serikali na imejipanga vyema kupokea na kutatua changamoto walizonazo wananchi za huduma ya maji.

Ameongeza kuwa katika kampeni hii ya DAWASA mtaa kwa mtaa, Mamlaka itaenda kuhakikisha inafuatilia kwa ukaribu kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, kuhakikisha wananchi wanaufahamu juu ya usomaji wa mita za maji.

Naye Diwani Kata ya Kunduchi Mhe. Michael Urio ameitaka DAWASA kuongeza mawasiliano na Taasisi nyingine ikiwemo Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) hususani wakati wa utekelezaji wa miradi kwa lengo la kunusuru uharibifu wa miundombinu ya maji ikiwemo mabomba ya barabarani.







Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages