MAMLAKA ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama imefanya operesheni maalum mkoani Morogoro kwa muda wa siku tisa katika vijiji vya Nyarutanga, Lujenge na Mafumbo vilivyopo wilaya za Morogoro vijijini na Kilosa.
Katika vijiji vya mafumbo na Lujenge Mamlaka imeteketeza jumla ya ekari 1,165 za mashamba ya bangi na kukamata kilogramu 102 za mbegu za bangi.
Aidha, katika operesheni iliyofanyika kijiji cha Nyarutanga watu 6 wakiwa na kilogramu 342 za bangi wamekamatwa na watafikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Akizungumza mara baada ya utekelezaji wa mashamba hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mashamba ya bangi yaliyoteketezwa yamelimwa pembezoni mwa mto Mbakana, Misigiri na Mgeta kwenye eneo la akiba la hifadhi ya Taifa Mikumi.
“Uharibifu mkubwa sana wa mazingira umefanyika katika eneo hili ambapo miti imekatwa ili kupata eneo la kulima bangi na hivyo kuharibu uoto wa asili. Pia uharibifu uliofanyika katika eneo la akiba la Mikumi unaharibu ikolojia ya eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa uoto wa asili na ikizingatiwa mito hiyo inatiririsha maji katika bwawa la Mwakimu Nyerere linalotegemewa kwa uzalishaji wa umeme” amesema Lyimo.
Kadhalika, amewashukuru sana wananchi hususan vijana waliojitolea kushiriki katika zoezi zima la utekelezaji wa mashamba ya bangi pamoja na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha mamlaka kuweza kufanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi na kutokomeza dawa za kulevya nchini Tanzania.
“Sisi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tutajitahidi kutekeleza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha kwamba tunamaliza tatizo la dawa za kulevya nchini ikiwemo mashamba ya bangi, mashamba ya mirungi pamoja na kudhibiti kemikali bashirifu na matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya kutumika kama mbadala wa dawa za kulevya. Hivyo, wote watakaojihusisha na uzalishaji, matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya tutawakamata” amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.
Hata hivyo, amewaomba wananchi wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine kushirikiana na Mamlaka kupiga vita kilimo cha bangi na aina nyingne za dawa za kulevya kwa ujumla kwani operesheni hizi ni endelevu.
Kwa upande wake Saidi Mijinga mkazi wa Kisaki, na mmoja wa vijana waliojitolea kishirikiana na Mamlaka kufyeka mashamba ya bangi amesema, eneo lililotumika kulima bangi ni kubwa sana, endapo lingetumika kulima mazao mengine wananchi wangenufaika kwani mazao hayo hulimwa bila kificho na kuuzwa kwa uwazi jambo ambalo lingewaletea faida ya chakula na kipato na hivyo, kuondokana na changamoto za njaa kwani kuna wakati wanakumbwa na tatizo hilo.
“Ninawashauri wanaolima bangi waache hii tabia walime mazao mengine ili tufaidike wote kwa sababu kuna kunde, mahindi, choroko, maharage na mbaazi yote haya yanakubali. Hili eneo ni kubwa sana linaweza likatulisha sisi kijiji na kuifanya njaa isiwe gumzo. Kwani kuna muda unafikaga vyakula hakuna zipo bangi tu, Sisi hatuwezi kula bangi” amesema.