Breaking

Wednesday, 14 August 2024

WANAGDSS WAJENGEWA UELEWA KUHUSU KANUNI ZA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA 2024


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WADAU wa Semina za Jinsia na Maendeleo wamejengewa uelewa kuhusu kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na kuzichambua kwa mtazamo wa kijinsia hasa zile ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), Mwasilishaji Deogratius Temba amesema wananchi wanatakiwa kuelewa kanuni za uchaguzi ili waweze kushiriki vizuri kwenye mchakato wa uchaguzi kwa kuhakikisha wanafuata taratibu za uchaguzi.

Amesema sehemu ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 inaeleza kuhusu matangazo ya uchaguzi, usimamizi wa uchaguzi, na maelekezo muhimu kuhusu uchaguzi ambapo muhimu kuangalia jinsi kanuni hizi zinavyowezesha ushiriki wa wanawake na kuzingatia haki za kijinsia.

Amesema miongoni mwa kanuni hizo imeeleza kuhusu uandikishaji wa wapiga kura utaanza siku arobaini na saba kabla ya uchaguzi, na utachukua siku kumi.

"Uandikishaji ukifanyika kwa muda mrefu na sehemu inayofikikakirahisi, wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu, ikiwa hatuzingatii muda na mazingira kundi kubwa litakaloshindwa kujiandikisha ni wanawake". Amesema

Aidha amewataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ili waweze kuonesha uwezo wao wa kuongoza na kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wa wadau wa semina za jinsia na maendeleo wamesema kupitia uelewa ambao wamepitishwa kuhusu kanuni za uchaguzi, watahakikisha wanajitokeza kwa wingi kwenye mchakato wa uchaguzi kuanzia kugombea nafasi mbalimbali na pia kushiriki kupiga kura.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages