Breaking

Tuesday, 6 August 2024

VIFARANGA VYA KUKU VYAPATA MUAROBAINI KATIKA UKUAJI

Mashine inayosaidia katika uleaji wa vifaranga vya kuku iliyobuniwa na Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Na Nora Damian

Wafugaji kuku wa kisasa na kienyeji sasa wataondokana na adha ya kupata hasara kutokana na vifo vya vifaranga baada ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kubuni teknolojia inayosaidia kulea vifaranga.

Teknolojia hiyo ambayo pia inatoa taarifa kwa mfugaji iwapo chakula au maji yameisha imebuniwa na mwanafunzi wa mwaka wa nne katika fani ya Uhandisi wa Mitambo, George Luambano.

Akizungumza Agosti 5,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Luambano ambaye pia ni mfugaji kuku amesema mashine hiyo inamsaidia mfugaji kulea vifaranga katika kipindi ambacho wanahitaji chanjo na matunzo mengine muhimu ili kuhakikisha wanakuwa na afya njema.

“Mashine hii ni zao la vitu ninavyojihusisha navyo kwa sababu mimi ni mfugaji, baada ya kuona napata hasara na wafugaji wengine wanapata hasara wakati wa kufuga vifaranga, lilinijia wazo nitatue tatizo. Nimetengeneza mashine kuhakikisha kila mfugaji anaweza kukuza vifaranga na kupunguza vifo ili tupate vifaranga wengi na nyama nzuri.
“Mashine inasaidia kulisha kuku, kuwapa maji kwa muda maalumu, kuwapa joto na unyevunyevu. Inaweza kumsaidia mfugaji kutopoteza muda wa kuangalia kama maji au chakula kipo…chakula au maji yakipungua huwa inatoa taarifa mtu anakuja kuongeza,” amesema Luambano.

Amesema mashine hiyo inatumia taa za joto na hata likipungua zinaendelea kuwaka na ikifika linalohitajika kwa kuku (nyuzi 33) zitazimika huku pia kukiwa na feni inayoingiza hewa ndani.

Amesema kwenye maji kuna kifaa kinachopima kina cha maji na ikitokea kimepungua zaidi itatoa taarifa na mfugaji ataongeza.

“Matatizo ya ufugaji hayaishi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kiuchumi na mabadiliko ya teknolojia kwahiyo, tatizo linapotokea ni bora kulitatua mapema,” amesema.

Mwanafunzi huyo amesema tayari amepata maombi kutoka kwa wafugaji katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuwatengenezea mashine hiyo ambayo inatatua tatizo ambalo kila mfugaji linamkuta.

Naye Ofisa Uhusiano Mkuu wa NIT, Tulizo Chusi, amesema wana kitengo cha kuendeleza bunifu ambacho kinalenga kuhakikisha bunifu zinazobuniwa na wanafunzi zinaifikia jamii.
Ofisa Uhusiano Mkuu wa NIT, Tulizo Chusi, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema chuo kinafanya kazi ya kuendeleza bunifu za vijana hao na kuziingiza sokoni na tayari kuna ambazo zimesajiliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa ajili ya kwenda kwa walaji.

“Tuna kitengo cha kuendeleza bunifu zinazobuniwa na wanafunzi na tuna wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba bunifu haziishii chuoni bali zinaifikia jamii,” amesema Chusi.

Ofisa huyo amesema dirisha la udahili bado liko wazi na kuwakaribisha wananchi waweze kujiunga na kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages