NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetenga fedha katika Bodi ya Maktaba Tanzania kwa ajili ya ununuzi wa vitabu ili kuwezesha watanzania kupata vitabu na kujenga tabia ya usomaji.
Hayo yameelezwa Agosti 02, 2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Riwaya chenye jina Tangled Web kilichoandikwa na Euanice Urio.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya kuchapisha, kununua na kusambaza katika shule na maktaba vitabu vya Washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu
"Serikali bado inahimiza uandishi na usomaji wa vitabu na ndio maana ilianzisha Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo inahusisha uandishi wa riwaya, mashairi, hadithi fupi na za watoto katika lugha ya kiswahili" amesema Waziri wa Elimu.
Nae Mkurungezi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amewataka waandishi wa vitabu nchini kuviwasilisha TET ili vipatiwe ithibati kwa ajili ya kutumika shule.
Pamoja na hayo Dkt. Komba amesema hayo Agosti 02, 2024 Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Kitabu cha Mwandishi Euanice Urio kiitwacho Tangled Web ambapo amesema utaratibu wa kupeleka vitabu TET ni wa kawaida ili kuona kama vina maudhui yanayoweza kutumika shuleni na kuwajenga watanzania.
Dkt. Komba ameongeza kuwa vitabu vya riwaya vya Kiingereza na Kiswahili, hadithi za watoto na mashairi vinahitajika kwa wingi nchini na kwamba vitasaidia watoto wa kitanzania kusoma vitabu vilivyoandikwa na waandishi mahiri wa Tanzania.
"Katika mabadiliko ya mitaala imeanzisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya fasihi katika Kiswahili na Kiingereza kuanzia kidato cha tatu , hii ni nafasi kwa Waandishi kuandika vitabu vya kutosha ili kuwezesha watoto kutumia vitabu vilivyoandikwa na Waandishi Mahiri wa Tanzania" amesisitiza Dkt. Komba.
Kwa upande wake Mwandishi wa Kitabu cha Tangled Web Euanice Urio ameiomba Serikali kusaidia katika mnyororo wa Sekta ya Uandishi wa Vitabu ili kuwezesha upatikanaji wa vitabu na kuhamasisha usomaji nchini
Urio amesema kuwa changamoto kubwa katika sekta hiyo ni kuvipeleka sokoni kutokana na watanzania wengi kutokuwa na tabia ya usomaji wa vitabu.
Amesema kuwa ili kuondokana na changamoto hiyo ni kuhamasisha usomaji wa vitabu jambo ambalo ni gharama kubwa kwa waandishi kuweza kufanya hivyo na kuomba serikali isaidir katika upande huo.
"Ukweli usiopingika kwamba vitabu vinasaidia katika kutunza utamaduni na mila, historia ya nchi hivyo ni vyema serikali isaidie katika kuhakikisha kuna vitabu vilivyoandikwa na watanzania ili kupunguza usomaji wa vitabu vya nje ambavyo vimekuwa vikileta tamaduni zao ambazo wakati mwingine si sahihi kwetu" amesema Urio
Mwandishi huyo ameongeza kuwa watu wasipoandika vitabu itafika wakati nchi itapoteza historia na utamaduni kwa kuwa wananchi wanasoma vitabu vya nje.