Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amejidhatiti vyema katika kusambaza miradi ya umeme mijini na vijijini na sasa umekuwa si anasa tena kutokana na wananchi kuutumia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Agosti 16, 2024 wakati akizindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Mpingi Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
"Ni dhamira ya Mhe. Rais kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 nchini vinapata umeme, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), tumebakisha chini ya Vijiji 151 kuvipelekea umeme na kazi inaendelea." Amesema Mhe. Kapinga
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa Serikali inakwenda kufuta historia ya Vijiji vya Tanzania kutokuwa na umeme kutokana na Vijiji vyote kwenda kufikiwa na nishati hiyo.
Aidha, kutokana na kuelekea kukamilika kwa upelekaji wa umeme kwenye Vijiji, Kapinga amesema sasa Serikali imeelekeza nguvu katika usambazaji wa umeme kwenye Vitongoji.
Amewahakikishia Watanzania kuwa, Serikali itaendelea kupeleka huduma ya umeme katika maeneo yote nchini ili watanzania waweze kuboresha shughuli za kiuchumi.
Awali, Mha.Robert Dulle ambaye ni Msimamizi wa miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Ruvuma alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwa kuunganisha kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.
Aidha, amewaasa wananchi kutunza miundombinu ya umeme hasa kipindi cha utayarishaji wa mashamba ambapo miundombinu mingi huathirika kwa kuchomwa moto.