Breaking

Saturday 31 August 2024

ORYX GAS YAJIVUNIA KUWAFIKIA MAMA NA BABA LISHE ZAIDI 12000

KAMPUNI ya Oryx Gas imetoa mitungi na majiko yake 1000 kwa washiriki wa mashindano ya kupika kwa gesi ya Oryx mkoani Mbeya lengo la kuwawezesha kurahisisha shughuli zao za mapishi huku Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akieleza Serikali imewataka wadau wa gesi kuangalia uwezakano wa kuwa na gesi ambayo Mwananchi atanunua kidogo kidogo kila siku.

Mashindano hayo ya kupika kwa gesi yaliyofanyika kuanzia Agosti 27 na kuhitimishwa leo Agosti 31,2024 yameandaliwa na Mbunge wa Mbeya Mjini Dk.Tulia Akson kupitia taasisi yake ya Tulia Trust a kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania.

Akizungumza wakati akihitimisha mashindano hayo,Naibu Waziri Judith Kapinga aliyekuwa mgeni rasmi amesema Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na lengo ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati mbadala katika kupikia.

" Moja ya maombi ya wananchi kwa wadau wa gesi ni kupunguzwa kwa bei ya gesi ambayo kwa sasa ni kubwa.Tunashauri wadau katika sekta hii ya gesi tengenezeni mfumo ambao utawezesha Mwananchi kununua gesi kidogo kidogo kwa siku badala ya kutoa fedha nyingi kwa wakati mmoja,"amesema.

Amesisitiza kukiwa na uwezo wa gesi kununuliwa kidogo kidogo anaamini wananchi wengi watatumia gesi na hivyo kusaidia kupunguza Kasi ya uharibu wa mazingira lakini pia kulinda afya za wananchi.

Naibu Waziri Kapinga amesema katika mwaka wa fedha uliopita wamegawa mitungi kwa wananchi na mwaka huu wa fedha wametenga fedha kwa ajili ya kuendelea kugawa nishati mbadala ya kupikia kwa wananchi huku akisisitiza kuwa kinara wa Nishati Safi Rais DK.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuona asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia nishati hiyo.

Kuhusu tamasha hilo la mapishi , Naibu Waziri Kapinga amempongeza Dk.Tulia Ackson kuandaa mashindano hayo makubwa na kushirikisha Mama na Baba Lishe 1000 kushindana kupika kwa gesi kwani yamekuwa ya mfano na yametumika kutoa elimu ya nishati na utunzaji mazingira.

Pia amesema kumekuwa na dhana kupika kwa kuni na mkaa ndio chakula kinakuwa kitamu lakini ukweli chakula kinachopikwa kwa nishati mbadala kama gesi ni kitamu na kinaladha.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Oryx kwa kuendelea kuishika mkono Serikali katika kusaidia kuhamasisha nishati safi ya kupikia,wanafanya kazi nzuri na wamekuwa wakifika kila mahali wakigawa mitungi na majiko yake kwa jamii.

Kwa upande wake Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dk.Tulia Ackson amesema kuna kila sababu ya kuendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye Afrika inatambua kama kinara wa nishati safi ya kupikia huku akiwahamiza wananchi kutumia nishati safi ambayo ni salama kwa afya na mazingira.

"Tumefanya mashindao haya ya kupika kwa gesi kwa Baba na Mama Lishe  kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais DK.Samia Suluhu Hassan ambaye kama mnavyofahamu yeye ndio kinara wa nishati safi ya kupikia Afrika na sasa ametambuliwa duniani kote yeye ndio kinara wa nishati safi ya kupikia.

"Pia tunapofanya mambo kama haya ya kufundishana kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na kuachana na nishati isiyosalama tunaamini mtahamasika  na kutumia nishati mbadala mnapotipikia vyakukula katika migahawa na vijiwe vyenu,hivyo tutakuwa tumelinda mazingira.Majiko na mitungi ya gesi ambayo mmepewa na wadau Wetu Oryx ikawe chachu ya ninyi kukua kutoka hatua moja hadi nyingine,"amesema.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Oryx ambao wamekuwa wakiungana naye katika matukio mbalimbali yanayohusu wananchi na hasa kwa kuendelea kuwezesha jamii kupata mitungi na majiko ya Oryx.

"Tunawashukuru kwasababu mbali ya kutoa majiko 1000 kwa Baba na Mama Lishe wote walioshiriki mashindano haya pia mmetoa na mitungi mikubwa na majiko yenye sahani mbili kama zawadi kwa washindi hivyo wanakwenda kukuza biashara zao."

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema lengo kuu la mashindano ya mapishi ni kuhamasika matumizi ya nishati safi kwa lengo la kulinda mazingira ambayo yamekuwa yakiharibiwa kwasababu ya kukata kuni na mkaa.

"Kwa miaka zaidi ya 15 iliyopita upatikanaji wa nishati ya kupikia umekuwa ukipangwa na kujadiliwa lakini hivi sasa Serikali inayoongozwa na Rais DK.Samia Suluhu Hassan amekuwa na hamasa kubwa ya kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

"Oryx Gasi tunaamini kupika kwa gesi kunakwenda kusaidia kulinda mazingira sambamba na kupunguza muda mwingi kwa wanawake kuwa porini kutafuta kuni na mkaa kwa ajili ya kuanda chakula.Pia kupika kwa gesi kutasaidia kuwalinda wanawake dhidi ya wanyama wakali walioko misitu lakini kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatilii ambavyo wanakutana navyo wakiwa porini."Amesema Benoit.

Ameongeza pamoja na kusaidia makundi mbalimbali kuyawawezesha kupata mitungi ya gesi ya Oryx lakini wanajivunia kuwafikia Mama na Baba Lishe zaidi ya 12000 ambao wamepata elimu ya matumizi salama ya kupika kwa gesi sambamba na kuwapatia mitungi midogo na mikubwa kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli za mapishi kwa urahisi na kuwa salama kiafya,"amesema.

Pamoja nayo hayo amesema kubalika kutoka kutumia kuni na mkaa hadi kupika kwa gesi kunatafsiri kubwa ya kwamba nchi imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo na kusisitiza oryx Gas itaendelea kuhamasisha nishati safi ili kufikia malengo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi.

Awali akizungumza kwa niaba ya Machifu Mkoa wa Mbeya, Chief Chief Rocket Mwashinga amewaomba viongozi wa Serikali na wadau wa gesi kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya gesi ili wananchi waweze kumudu gharama kwani kwa sasa bado iko juu.

"Gesi ipunguzwe bei ili wananchi tuokoe mazingira kwani bei ikiwa kubwa wataendelea kushambulia misitu na kuharibu mazingira.Mazingira ni muhimu sana na sisi Machifu tuko maeneo ya pembezoni mwa Mkoa ambako kuna miti niwahakikishie machifu na viongozi wote wa kimila nchini tunaouwezo mkubwa wa kulinda mazingira,kikubwa tunaomba tuwezeshwe."

Kwa upande wao baadhi ya Mama na Baba Lishe walioshiriki mashindano ya kupika kwa gesi wamesema kupitia mashindano hayo wamenufaika na mafunzo waliyoyapata sambamba na kuelezwa umuhimu wa kutunza mazingira na wanatoa shukrani kwa waandaaji wakiongozwa na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dk.Tulia Ackson. 
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages