Breaking

Saturday, 3 August 2024

KATIBU MKUU AFURAHISHWA NA MAANDALIZI YA TVLA NANENANE

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kituo cha Dodoma Dkt. Japhet Nkangaga kuhusiana na huduma zinazotolewa TVLA kwa wafugaji na wadau kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma alipotembelea kujiridhisha na maandalizi ya Maonesho hayo tarehe 2 Agosti, 2024.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ameridhishwa na maandalizi ya Maonesho ya Nanenane yaliyofanywa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa lengo la kutoa elimu kwa wafugaji na wadau mbalimbali kuhusiana na huduma zinazotolewa na TVLA kwenye maonesho ya Nanenane kitaifa yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma kuanzia tarehe 1 agosti 2024 hadi 8 Agosti, 2024

Prof. Shemdoe amekagua huduma hizo tarehe 2 Agosti 2024 alipotembelea taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kujiridhisha na huduma zitakazotolewa kwa Wafugaji, Wavuvi na wadau mbalimbali watakaotembelea Maonesho hayo.

Huduma zilizokaguliwa na Katibu Mkuu kwenye banda la TVLA ni pamoja na elimu ya uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama, elimu ya matumizi sahihi ya Chanjo za Mifugo, elimu ya uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, elimu ya usajili na uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya Mifugo, elimu ya utafiti wa magonjwa ya wanyama pamoja na elimu kuhusiana na mafunzo kwa wataalamu wa Mifugo inayotolewa na TVLA.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania inashiriki Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa elimu ya huduma bora za maabara za Veterinari, kutoa elimu ya utafiti juu ya magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa hayo ndani na nje ya Tanzania.

Vilevile TVLA imejipanga kuimarisha uzalishaji endelevu katika sekta ya Mifugo, Usalama wa Chakula na kuchangia kwenye Uchumi wa Taifa kupitia utoaji wa huduma bora zenye gharama nafuu za Uchunguzi na Utambuzi, uzalishaji wa bidhaa za veterinari na kufanya tafiti za magonjwa ya Mifugo na wadudu waenezao magonjwa hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akikagua Msimbo upau (barcode) ya Chanjo ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi kutoka kwa Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kituo cha Dodoma Dkt. Japhet Nkangaga alipotembelea banda TVLA kujiridhisha na maandalizi pamoja na huduma zinazotolewa kwa wafugaji na wadau kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma tarehe 2 Agosti, 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtafiti Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Shabani Motto kuhusiana mashine ya uchunguzi wa kutambua uwepo wa vinasaba (Real time PCR) alipotembelea banda la TVLA kujiridhisha na maandalizi pamoja na huduma zinazotolewa kwa wafugaji na wadau kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma tarehe 2 Agosti, 2024.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages