Breaking

Saturday 31 August 2024

FAWE ZANZIBAR, UN WOMEN ZINAVYOWEZESHA WANAWAKE KUFIKIA KIZAZI CHENYE HAKI NA USAWA KIUCHUMI

 

KATIKA jitihada za kuhakikisha Tanzania inafanikisha utekelezaji wa malengo manne ya kizazi chenye usawa, Jukwaa la Wanawake Wanaelimu wa Afrika, Zanzibar (FAWE Zanzibar) inawezesha wanawake Zanzibar kukabiliana na vikwazo kiuchumi.


Kwa kushirikiana na UN Women Tanzania, FAWE Zanzibar inachangia ufikiaji wa malengo hayo kupitia utekelezaji wa  Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa wa Kuharakisha Maendeleo ya Kiuchumi kwa Wanawake Vijijini (JPRWEE) unaolenga kuhakikisha ustawi wa wanawake vijijini na haki zao.


Utekelezaji wa mpango huo unaenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa wanawake ili kuwasaidia  kupata ujuzi wa biashara, elimu ya kifedha, pamoja na fursa za kupata mikopo ili kuanzisha na kukuza biashara zao.


Miongoni mwa mafanikio yaliyoelezwa na wanufaika wa mradi huo ambao unatekelezwa Mkoa wa Kusini Unguja ni kuongezeka kwa ajira, hali iliyoboresha kipato cha kaya na kupunguza utegemezi kwa waume. 


Walisema mradi huo umewawezesha wanawake wengi kuanzisha biashara ndogo ndogo, kama vile kuuza bidhaa za kilimo, ushonaji, na uzalishaji wa bidhaa za nyumbani kama sabuni na mishumaa.


Si wanawake tu walionufaika na uwepo wa mradi huu, hata kwa wanaume pia mradi huu umebainika kuwa ufunguo wa kuifikia haki na usawa wa kiuchumi.


Assaa Hassan Khamis, ni mwanakikundi cha Upishi, SUBIRA INA MALIPO kutoka shehia ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja alisema, “mafanikio ninayojivunia ni kupata mafunzo ya upishi ambayo yamenisaidia katika kujiajiri mimi mwenyewe na kumsaidia mke wangu majukumu ya kupika akiwa na tatizo.” 


Nae Mwanakombo Nyange Shamata kutoka kikundi cha UROA SACCOS, alisema wamepata mikopo ambayo imewasaidia kununua vifaa vya ukulima wa Mwani ambao ndio wanautegemea kwa kuendeshea maisha yao ya kila siku.


“Tumepata mafanikio makubwa katika mradi huu kwani tumepata mikopo ambayo imetufanya tununue vifaa vya ukulima wa Mwani ambao ndio rasilimali ya uchumi wetu,” alieleza Mwanakombo huku akitabasamu.


Kwa upande wa Shida Hassan Mambo, kutoka kikundi cha TUPENDANE kilichopo Uroa wilaya ya Kati Zanzibar, alisema kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, wanawake wengi wameweza kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi. 


Aidha alibainisha, wamejifunza mbinu za kujiwekea akiba, kuweka kumbukumbu za kifedha, na kupanga matumizi yao vizuri, hali iliyosaidia biashara nyingi kukua.


“Mradi umetusaidia sana sisi wanawake kufanya shughuli zetu za kiuchumi ikiwemo kuweka na kukopa jambo lililotusaidia kujikwamua na changamoto ya kifedha tunapopatwa na matatizo,” alisema mwanakikundi huyo.


Licha ya juhudi kadhaa zinazochukuliwa. Lakini Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto ya soko la Mwani.


“Serikali imesema kilo ya mwani inunuliwe kwa shilingi 1,000 lakini wanunuzi hununua kwa Shilingi 700. Hatupati chochote zaidi ya maumivu,” alisema Arabia Fauzi Pandu mwanakikundi cha Mwani cha USALAMA WETU kutoka Jambiani Wilaya ya Kusini.


Afisa tahmini na ufatiliaji FAWE Zanzibar, Shaban Suleiman alisema  mradi unawawezesha wanawake wa vijijini kiuchumi ili kuona wanapata maendeleo  ya kiuchumi katika maisha yao.


“Tumewapatia elimu ya ujasiriamali na elimu ya biashara ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi katika kujikusanya kwa pamoja na tumewahamasisha kuchukua mikopo serikalini kwa maendeleo yao zaidi,” alisema Shaaban.


Silvia Lanzarini, Afisa Ufuatiliaji na Mtaalam wa Programu kutoka UN Women akitembelea wanufaika hao aliwashauri wajasiriamali wanawake kuweka akiba ya fedha kwenye vikundi vyao ili waweze kupata mikopo zaidi itakayosaidia kutatua changamoto ndani ya vikundi vyao na jamii inayowazunguka.


“Nimefurahi kukutana nanyi katika kuona mafanikio na changamoto zenu katika mradi huu, ni matumaini yangu mafanikio muliyoyapata munayafurahia,” Silvia aliwaeleza huku akionesha kufurahishwa na juhudi zao.


Programu ya Kizazi Chenye Usawa (2021- 2026) inajumuisha afua nne ikiwemo kuanzisha na kuendeleza vituo vya malezi na makuzi ya watoto; kuongeza uwekezaji katika usambazaji wa maji, umeme na nishati mbadala yenye kutunza mazingira na matumizi ya teknolojia yenye gharama nafuu; kuongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara na urasimishaji wa biashara za wanawake; na kuboresha upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa soko la ndani na nje.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages