Breaking

Tuesday, 20 August 2024

BARRICK YAKABIDHI GAWIO LA MRAHABA VIJIJI 5 WILAYANI TARIME


Kampuni ya Barrick nchini yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals kupitia mgodi wake wa North Mara, imekabidhi gawio la mrahaba wa shilingi bilioni 1.1 kwa vijiji 5 wilayani Tarime, ambapo katika robo ya pili ya mwaka jana mpaka robo ya kwanza ya mwaka huu pia ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.2 .

Mgao huo umetolewa kwa vijiji 5 vya Genkuru, Nyamwanga, Nyangoto, Kerende na kewanja ambayo vilikuwa vikimiliki maeneo yenye leseni za uchimbaji wakati mgodi unaanzishwa na kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mines ambayo sasa ni North Mara Gold Mine kwenye shimo la Nyabigena.

Hafla ya kukabidhi hundi za mgao wa mrahaba kwa viongozi wa vijiji hivyo ilifanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Igwe wilayani Tarime na kuhudhuriwa na wanavijiji hivyo,wajumbe wa kamati ya Madini ya Bunge, Viongozi wa Serikali, Madiwani, wenyeviti wa vijiji, wafanyakazi wa Barrick North Mara na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde.

Akiongea katika Hafla hiyo, Waziri Mavunde, alisema Serikali itaendelea kusimamia kwa umakini sekta ya madini nchini ili iweze kuchangia ukuaji wa pato la Taifa sambamba na kuwanufaisha wananchi hususani wanaoishi maeneo yanayozunguka migodi kupitia tozo mbalimbali za kisheria ikiwemo fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR) ambazo zimekuwa zikitumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.

“Katika miaka ya karibuni sekta ya madini imetoa mchango mkubwa kwa pato la taifa hadi kufikia na katika mwaka wa fedha uliomalizika iliweza kuchangia kiasi cha bilioni 753 na hii inatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyojengwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan”,  alisema.

Alisema Wizara ya Madini itahakikisha inayafanyia kazi malalamiko ya wananchi wanaoishi maeneo ya migodi hususani yanayohusiana na malipo ya fidia, ukosefu wa huduma muhimu za kijamii na alitoa rai kwa viongozi wa Serikali waliopo maeneo hayo kukutana na wananchi na mwekezaji kwa ajili ya kupata suluhusisho la malalamiko hayo pia aliitaka Mgodi wa Barrick North Mara, uangalie uwezekano wa kusaidia wachimbaji wadogo waweze kujikwamua kiuchumi sambaba na kuwekeza zaidi katika mradi wa kilimo Biashara kwa ajili ya kupunguza changamoto ya ajira katika makundi mbalimbali ya jamii wilayani Tarime.

Kwa upande wake, Meneja wa Barrick Nchini,Melkiory Ngido,aliishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na aliahidi kuwa kampuni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi sambamba na kufanyia kazi maagizo na ushauri wa viongozi wa Serikali ili kujenga mahusiano mema.

Awali akiongea katika hafla hiyo,Meneja Mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara ,Apolinary Lyambiko, alisema kampuni imeendelea kutoa gawio la mrahaba kwa vijiji 5 ambavyo vilikuwa vikimiliki maeneo yenye leseni za uchimbaji wakati mgodi unaanzishwa ambapo kufikia robo ya kwanza ya mwaka ya mwaka huu kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kililipwa na malipo ya robo ya pili ni kiasi cha shilingi bilioni 1.1.

Lyambiko, alisema malipo mengine ambayo yamelipwa na mgodi kwa jamii na Serikali kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 ni kiasi cha shilingi bilioni 69 ambazo zimelipwa kama mirahaba kwa wamiliki binafsi wa leseni zilizomilikishwa kwa mgodi,michango kwa North Mara Trust Fund kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kupata elimu,Tozo za usharu wa huduma (Service Levy kwa halmashauri ya Wilaya ya Tarime, na fedha za wajibu wa wamiliki wa leseni za madini kwa jamii (CSR).

Akielezea changamoto mbalimbali ambazo mgodi unakutana nazo alisema bado kuna uvamizi haramu mgodini sambamba na mlundikano wa kesi ambazo nyingine hazihusu mgodi ambazo zimekuwa zikitumia muda mwingi kuzifuatilia sambamba na gharama.

Akiongea kwa niaba ya viongozi wa vijiji vilivyopata gawio la mrahaba,Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto,Mwita Musegi, aliishukuru kampuni ya Barrick kwa kutoa fedha hizo na kuahidi kuwa zitasimamiwa vizuri kuhakikisha zinafanikisha kutekeleza miradi ya kuboresha maisha ya wananchi.
Viongozi wa vijiji vilivyopata gawio la mrahaba wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde na viongozi wa Barrick na Serikali mkoani Mara
Viongozi wa vijiji vilivyopata gawio la mrahaba wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde na viongozi wa Barrick na Serikali mkoani Mara
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde,akiongea katika hafla hiyo
Meneja Mkuu wa Barrick North Mara,Apolinary Lyambiko akiongea wakati wa hafla hiyo
Meneja wa Barrick Nchini,Melkiory Ngido akiongea na wananchi katika hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick North Mara katika hafla hiyo
Viongozi mbalimbali walikuwepo pia
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akipata maelezo ya mradi wa kilimo biashara wa kuwezesha wananchi ulioanzishwa na kufadhiliwa na mgodi wa Barrick North Mara
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages