Breaking

Tuesday, 13 August 2024

ACHOMA NYUMBA MUMEWE NA WATOTO WAKIWA NDANI



Wakazi wa kijiji cha Kathaia kaunti ya Embu wamekumbwa na mshtuko baada ya mwanamke kudaiwa kuteketeza nyumba yake ya vyumba vitatu kufuatia mzozo unaoshukiwa kuwa wa kinyumbani. 

Beatrice Mueni anaripotiwa kuwasha moto huo huku mumewe Martin Njeru Gicovi na watoto wao wawili wenye umri wa miaka 12 na 8 wakiwa wamelala ndani.

Gicovi alisimulia kisa cha Jumapili, Agosti 11, akisema kwamba aliamshwa na moshi huo na kufanikiwa kutoroka kupitia dirishani akiwa na watoto hao.

"Nilikuwa nimelala fofofo nilipohisi harufu ya kitu kinachoungua. Niliamka na kukuta nyumba inawaka moto. Ilinibidi kuvunja dirisha ili kutoroka kisha nikarudi kuokoa watoto wangu," Gicovi aliambia Citizen Digital.

Mueni alidai kuwa alikuwa nje akianua nguo nje moto ulipoanza.

Kisha akaenda Ena Police Post kuripoti madai ya kushambuliwa na mumewe huku majirani wakijaribu kuzima moto huo.

Hata hivyo majirani waliojawa na hasira walimfuata hadi kituo cha polisi wakitaka kueleza kuhusu kisa hicho, hali iliyopelekea kukamatwa kwake.

Huku hali ya wasiwasi ikiongezeka, Mueni alikiri kuwasha moto huo kimakusudi ili kuharibu mali yake.

Polisi wametembelea eneo la tukio, kutathmini uharibifu, na kuanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo la kuhuzunisha.

Gicovi alidai kuwa uharibifu uliosababishwa na moto huo ulikuwa takriban KSh 90,000.


Source: Tuko News 
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages