Breaking

Tuesday, 30 July 2024

ZIARA YA BALOZI NCHIMBI YAFYEKA ACT, CUF NA CHADEMA KUSINI


Ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, inayoendelea katika mikoa ya Kusini, akianzia Mtwara na sasa yuko Lindi, imewahamisha viongozi waandamizi wa vyama vya ACT Wazalendo, CUF na Chadema walioamua kujiunga CCM leo, wakisindikizwa na mamia ya wanachama waliorejesha kadi zao za vyama vya zamani kwa kasi kubwa kwenye mkutano wa hadhara.

Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mpilipili, Lindi mjini, ukiwa ni mwendelezo wa ziara ya Balozi Nchimbi, amewapokea viongozi hao waandamizi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mchinga Ndugu Hamidu Bobali akiambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Wanawake wa ACT Wazalendo Lindi Mjini Bi. Hawa Kipara, Meneja Kampeni wa Wabunge ACT Wazalendo Lindi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana CUF Lindi Issa Sapanga, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Mwenyekiti wa Wanawake Chadema Lindi Mjini pamoja na Wanachama 250 wa ACT Wazalendo.

Wakati akikabidhi kadi yake ya ACT na kujiunga CCM, Ndugu Bobali amesema;

“Nimeishi miaka 20 nje ya CCM ambako niliaminiwa sana katika ngazi tofauti ndani ya CUF na ACT Wazalendo hadi kuwa Waziri Kivuli wa Maji lakini nikiri niliyokuwa yanapigania Jemedari Samia ameyafanya kwa nguvu kubwa hivyo sina jinsi isipokuwa kujiunga CCM na kumuunga mkono. Kule upande wa pili tulikokuwa ametupiga kwenye mshono, hakuna tena agenda. Sasa hakuna kingine zaidi ya kazi nzuri za Dkt Samiana wenzangu hawa sasa tupo tayari kumsaidia.”

Naye Balozi Nchimbi akiwapokea wanachama hao wa vyama mbalimbali wakiongozwa na ACT Wazalendo amesema “karibuni huku wanachama wote ni sawa na mtapata ushirikiano mkubwa sana kuanzia sasa na kikubwa mmesema mmerudi sababu ya mambo makubwa yaliyofanywa na Dkt Samia nawapongeza kwa kuliona hilo mapema sasa tukaifanye Lindi ya kijani.”
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages