Breaking

Tuesday 2 July 2024

WAZIRI AWESO AWEKA MKAZO DAWASA KUUNGANISHA WANANCHI MAJI

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wananchi waliokidhi vigezo vya kupatiwa maunganisho ya majisafi wanapatiwa huduma hiyo kikamilifu.

Ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wa wananchi wa maeneo ya Tabata Segerea ulioitishwa kwa lengo la kusikiliza na kutafuta changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa maeneo hayo.

Ameeleza kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi kwa uhakika na kwa ufasaha.

Ameongeza kuwa ni haki ya kila mwananchi kuunganishiwa majisafi kulingana na utaratibu wa Kisheria wa Serikali uliopo.

"Utaratibu uliopo wa Serikali ni kwamba mwananchi aliyekidhi vigezo vya kuunganishiwa maji, anatakiwa afanyiwe maunganisho ya maji ndani ya siku saba za kazi," ameeleza Mhe. Aweso.

Mhe. Waziri ameiagiza Mamlaka kuhakikisha vifaa vya kufanya maunganisho ya majisafi kwa wateja vinapatikana kwa wakati ili wananchi waliokidhi vigezo waweze kufanyiwa maunganisho ya majisafi na wananchi waweze kunufaika na huduma.

"Kwa kuwa huduma ya maji ipo ya uhakika, pasiwepo na sababu yoyote ya mwananchi kukosa huduma, maana Serikali ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi za kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika," ameeleza Ndugu Aweso.

Ameitaka Menejimenti ya DAWASA kuongeza ufuatiliaji wa changamoto zinazosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA Mhandisi Evaristi Ndikilo amesema kuwa Bodi kwa kushirikiana na Menejimenti imezipokea changamoto zilizojitokeza na itakaa kupanga mikakati ya namna ya kusuluisha ili wananchi waweze kupata haki ya kuwa na majisafi.

Ameongeza kuwa Mamlaka imejipanga kikamilifu kuhakikisha katika mwaka huu mpya wa fedha kuhakikisha wananchi wa maeneo ya Kinyerezi, Segerea, Ubungo, Ukonga na Ilala wananufaika na maji kupitia mradi unaotekelezwa wa Dar es Salaam ya Kusini.






Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages