Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bwana Raymond Mndolwa, amewataka wahandisi na watumishi wa Tume kuheshimu, kusimamia na kutekeleza miradi kwa viwango na ubora.
Amesema ni aibu kwa taasisi kuwa na miradi isiyokidhi viwango hivyo hatakuwa tayari kuona miradi hiyo inaiangusha serikali na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Mndolwa amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na Menejiment, wasimamizi wa miradi, Wahandisi wa mikoa na wahakiki ubora wa miradi na baadhi ya watumishi.
Alisema, ni muhimu kila mmoja kujua serikali inafanya kazi kubwa kuwezesha miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi, hivyo ni muhimu usimamizi wake kuzingatia matokeo yenye ubora.
“Naomba kasimamieni miradi ni aibu kuwa na miradi isiyo na ubora, ni aibu kwenu na taasisi na tutaiangusha serikali na Chama ambacho kinatutaka tutekeleze Ilani.
“Mjue sitamuonea mtu lakini sitakuwa tayari kumvumilia yeyote asiyetekeleza wajibu wake, nitafanya mabadiliko mara kwa mara, lengo ni kuboresha utendaji na kuwa na ufanisi,”alisema.
Alitumia kikao hicho kusisitiza haja ya kuheshimu matakwa ya mifumo inayoanzishwa na serikali.
Mndolwa alisisitiza umuhimu wa watumishi hao kushirikiana na Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala (DAHRAM), ambaye ndiye mratibu wa utekelezaji wa shughuli za mifumo ya serikali ndani ya Tume.
Aidha, Bwana Mndolwa aliwakumbusha wahandisi wa umwagiliaji wa Tume kwa mikoa kuwa wasimamizi wa shughuli za utekelezaji wa majukumu ya tume ndani ya mikoa yao. Aliongeza kuwa wahandisi hao watapimwa kwa utekelezaji wa majukumu hayo.
Katika kuhakikisha ufanisi, Bwana Mndolwa alisisitiza watumishi wote kuheshimu sheria za utumishi, ikiwemo kufika kazini kwa wakati na kuvaa mavazi yenye hadhi. Kuhusu mabadiliko ya uongozi, Bwana Mndolwa alisema ofisi yake inalazimika kufanya mabadiliko ndani ya idara na vitengo vya Tume ili kuongeza ufanisi.
Alisisitiza kuwa mabadiliko hayo ni endelevu. Bwana Mndolwa pia aliwahimiza wahandisi kusimamia vyema majukumu yao ili kuepuka kuiangusha serikali na kutokwamisha utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa upande wa ushirikiano, Bwana Mndolwa aliwataka wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa kuwapa ushirikiano wahandisi wapya ili waweze kukua na kuimarika kiutendaji.
Katika kuhitimisha, Bwana Mndolwa alisisitiza umuhimu wa kuheshimiana, kujenga mahusiano mazuri kazini, watumishi kujali kazi za wenzao, na kuishi kwa upendo.
Alisema kufanya hivyo kutaimarisha hadhi ya taasisi ndani na nje ya Tume. Kwa upande wa mazingira ya utendaji kazi, Tume imenunua samani mpya za ofisi za mikoa na imejipanga kujenga ofisi mpya katika mikoa na wilaya, ikianza na wilaya 16 ili kuwawezesha watumishi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mwisho.