Breaking

Monday, 29 July 2024

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA MKOANI NJOMBE WAFIKIA ASILIMIA 88.3 - ENG RUTH

Bajeti ya Matengenezo na Maendeleo ya Barabara katika mkoa wa Njombe kwa Mwaka wa Fedha 2023-24, ni Shilingi Bilioni 11.583, ambapo katika fedha hizo Miradi ya Maendeleo ni Shilingi Bilioni 7.979, Miradi katika Ushoroba wa Kiuchumi Shs. Bilioni 2.0, Barabara Zilizopandishwa Hadhi Shilingi Bilioni 2.5 na Barabara zilizoathiriwa na Mvua ni Shilingi Bilioni 3.0.

Akizungumza kuhusu matumizi na utekelezaji wa fedha hizo Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua amesema kuwa utekelezaji wa Miradi unaendelea na umefikia Asilimia 88.3.

Amesema kuwa utekelezaji wa Miradi ya Kitaifa inayoendelea inahusisha Miradi ya Itoni – Ludewa – Manda Km 211.42 (Sehemu ya Itoni – Lusitu Km 50) yenye jumla ya Shs. Bilioni 120.901 ukitarajiwa kukamilika Disemba 13, 2024.

Mradi mwingine ni wa Isyonje – Kikondo – Makete Km 96.2 (Sehemu ya Kitulo – Iniho Km 36.3) na Ujenzi wa Mzani wa Igagala Shilingi Bilioni 82.635 ambapo kazi zote hizo zipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji ambapo ujenzi wake utakamilika Julai 11, 2026.

Ameitaja miradi mingine ambayo imeshakamilika kuwa ni Pamoja na Utekelezaji wa Miradi ya Kitaifa iliyokamilika ambayo inahusisha Barabara ya Njombe – Moronga Km 53.9, kwa gharama ya Shilingi Bilioni 136.268 uliokamilika Juni 2022 pamoja na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Moronga – Makete Km 53.5, uliotumia gharama ya Shilingi Bilioni 130 na ulikamilika Agosti 2022.

Mhandisi Ruth ameeleza kuwa TANROADS imekamilisha maandalizi ya Miradi itakayofanyiwa Upembuzi Yakinifu, na Usanifu wa Kina ya Kitulo II – Matamba - Chimala Km 42 na Matamba – Mfumbi Km 32, Bulongwa – Madihani – Kidope Km 22.16 na Madihani – Lufilyo Km 15.10, Njombe Bypass; Utekelezaji unatarajiwa kuanza Mwaka wa Fedha 2024-25 na mradi mwingine ni Ikonda – Lupila – Mlangali; ambao utekelezaji utaanza Mwaka wa Fedha 2024-25.

Kadhalika, Mhandisi Ruth amesema kuwa Katika Mwaka wa Fedha 2023-24, barabara ya wilaya iliyopanda hadhi na kuwa chini ya TANROADS ni moja yenye kilomita 34.40 ya Makoga – Kinenulo – Mdandu na zilizokasimiwa ni tano (5), zenye jumla ya kilomita 156.19 huku Barabara zingine zikiwa zimekasimiwa ambazo ni Barabara ya Bulongwa – Madihani – Kidope Km 22.16, Madihani – Lufilyo Km 15.10, Nkenja – Ikuwo – Usalimwani Km 42.70, Chimala – Matamba Km 22.10, na Kipengele – Kidugala – Mambegu Km 54.80.

Amesema kuwa barabara zilizokasimiwa na kupandishwa hadhi zimeingizwa katika mpango wa kila mwaka wa ukarabati na matengenezo huku akieleza kuwa maeneo yote yamepata wakandarasi na kazi zinaendelea.

Vilevile Mhandisi Ruth amesema kuwa mnamo Julai 12, 2024, barabara ya Kipengere – Lupila Km 42 ilipandishwa hadhi na kuwa barabara ya Mkoa ambapo barabara hii imeingizwa katika mpango wa Matengenezo wa Mwaka wa Fedha 2024 – 25.

Kuhusu ujenzi wa mizani amesema kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 4.628 zimetolewa na Rais Samia kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi 269.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages