Breaking

Sunday, 28 July 2024

UFUGAJI NYUKI WATOA AJIRA KWA VIJANA NCHINI

 

Na. John Bera 

Wakazi wa Kijiji cha Kisaki katika Manispaa ya Singida wameishukuru serikali kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki katika Ufugaji wa Nyuki ambayo yamewavutia watu wengi kuwekeza na kutoa ajira kwa vijana wengi.

Wananchi hao wameeleza hayo katika Kijiji cha Nyuki ambacho kimeweza kuzalisha ajira kwa vijana ambao wanajihusisha na ufugaji wa nyuki kibiashara na kuzalisha mazao mbalimbali ya nyuki.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Mwanzilishi, Mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kijiji cha Nyuki, Philemon Josephat Kiemi amesema kupitia ufugaji wa nyuki vijana wamepata ajira na wananchi wakipata huduma ya jamii bure.

Kiemi amesema akiwa anasoma kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Old Moshi ndipo alipoanza kuona kuwa asali ni sehemu ya biashara baada ya kuanza kuwauzia wanafunzi wenzake.

“Nilienda shule na asali na niliuza na kupata shilingi 200,000 wakati wazazi walikuwa wamenipa shilingi 75,000 kama fedha ya kujikimu na hapo ndipo akili ilipogundua kuwa hii ni sehemu ya biashara tangu kipindi hicho sikuomba tena fedha za matumizi nyumbani na nilijiajiri kupitia ufugaji wa nyuki", amesema  Kiemi.

Amesema biashara yake ya kuuza asali aliendelea hata akiwa anasoma Chuo Cha Kilimo SUA kwa kuanza kwenye nyumba za wafanyakazi wa chuo hicho.

“Hata nikiwa SUA nimeishi kwa kuuza asali na nta, hivyo taarifa nilizozipata na jitihada zilizokuwa zikifanywa na Waziri mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda zilinipa  ujasiri mkubwa wa kuingia kwenye biashara hii” ,amesema  Kiemi.

“Kwa sasa sina habari ya kuajiriwa na sijawahi kuajiriwa niliamua moja kwa moja kuja kujiajiri na ili niweze kuajiri wengine na mpaka sasa nimeajiri vijana 167 katika Kijiji cha Nyuki”,amesema Kiemi.

Amesema kwa mwaka jana wamegawa mizinga na vifaa vya kuvunia asali kwa wanakijiji 335, lengo likiwa  ni kuchangia uzalishaji wa asali kwa asilimia 50 ya mahitaji ya kiwanda ambacho kwa sasa kinachakata tani 450 huku mkakati ni kufikia tani 1000 ifikapo mwishoni mwa 2025.

“Wadau tunapaswa kushirikiana na kuona misitu na nyuki kuwa sehemu ya maisha ya watu kwa asilimia zaidi ya 60. Pia wahitimu wa vyuo vikuu wakiona msitu waone ni fursa kwa kuona msitu ni ofisi, dawa na ni chakula.”

Naye Afisa Utalii wa Kijiji cha Nyuki, Swaumu Mbwana amewataka vijana kutochoka katika kutafuta fursa ambazo zitawasaidia kuinua uchumi wao na kuendesha maisha yao.

 “Nikiwa kijana niliyehitimu shahada yangu, nyuki amenisaidia kupata ajira hapa Kijiji cha nyuki, lakini pia naweza kufanya biashara ya asali na vumbi la Singida (chavua ya nyuki) na kutengeneza mvinyo wa asali, hivyo vijana tujichanganye kwenye fursa mbalimbali ili tuweze kujikwamua kwenye janga la umasikini.”

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa sekta ya Ufugaji Nyuki inachangia ajira zaidi ya 2,000,000 hasa kwenye eneo la ufugaji nyuki, usindikaji na biashara ya mazao ya nyuki.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages